Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika utaondoa wanajeshi 3,000 zaidi kutoka Somalia.
"Maandalizi ya awamu ya pili ya kuondolewa kwa wanajeshi 3,000 wa ATMIS (Misheni ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia) kufikia mwisho wa Septemba yanaendelea," Luteni Jenerali Sam Okiding aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu siku ya Jumanne.
Kundi la kwanza la wanajeshi 2,000 wa kulinda amani waliondoka nchini mapema mwaka huu kama sehemu ya Mpango wa Mpito wa Somalia (STP), mwongozo ulioandaliwa na serikali ya Somalia na washirika wake kuhamisha jukumu la usalama kwa wanajeshi wa Somalia.
Okiding alisema ATMIS itaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Somalia, afisi ya msaada ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOS) na washirika wengine ili kuhakikisha uhamishaji wa majukumu ya usalama kwa Vikosi vya Usalama vya Somalia.
"ATMIS ingeweka hatua za kuepusha pengo la usalama wakati itakapoondoka Somalia mwishoni mwa Desemba 2024", aliongeza.
Vita dhidi ya Al-Shabaab
Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, ambao hapo awali ulijulikana kama AMISOM na kwa sasa ATMIS, ni ujumbe wa pande nyingi ulioidhinishwa na Umoja wa Afrika na kupewa mamlaka na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya kazi katika taifa hilo la Pembe ya Afrika tangu 2007.
Ujumbe huo unalenga kusaidia serikali ya Somalia katika vita vyake dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Kundi hilo la kigaidi limeongeza mashambulizi yao tangu Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alichaguliwa kwa muhula wa pili mwaka jana, kutangaza "vita vya hali ya juu" dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab.