Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito kwa nchi mbalimbali kuondoa lehemu ya ziada kwenye bidhaa za chakula, huku likiweka bayana kuwa mafuta hayo husababisha vifo vya watu milioni, kila mwaka./Picha: 

Na Sylvia Chebet

“Kula ni jambo la lazima; kula kwa akili ni sanaa,” mwanafalsafa François de La Rochefoucauld, aliwahi kusema.

Hata hivyo, bado hili ni jambo la kufikirika. Watu wengi duniani wamezoea kula vyakula vyenye lehemu nyingi, huku mkuu wa lishe ndani ya WHO Dkt Francesco Branca akisema kuwa kitendo hicho kinahatarisha afya.

Kati ya watu 300,000 hadi 500,000 hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na na kula vyakula vya aina hiyo, Dkt Branca anaiambia TRT Afrika.

“Vyakula hivi vinabidi viondolewe kwenye utaratibu wa milo kwani unasababisha magonjwa ya moyo,” anasema.

Matumizi yake husababisha kuziba kwa mishipa ya damu, na kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo na hatimaye vifo.

“Vyakula hivi havina manufaa yoyote ,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus

“Itoshe kusema kuwa vyakula venye lehemu huwa na chemikali zenye kuua, ni wakati muafaka kuviondoa kwenye utaratibu wetu wa milo ya kila siku,” aliongeza.

Vyakula vyenye lehemu ni vipi?

Linaweza kuwa jina gumu masikioni mwa watu, lakini vyakula hivi vinapamba majokofu na mafriji yetu. Hujulikana kwa ugumu wake na hutengenezwa viwandani au hata kupatikana kwa asili kwenye vyakula.

"Hutengenezwa katika mchakato wa kuimarisha mafuta ya kioevu ili kuzalisha kitu, kwa mfano, majarini na mchakato wa kiteknolojia unaotumiwa unafanywa kwa kuongeza hidrojeni kwenye mafuta ya kioevu."

Mbali na majarini na mafuta ya kupikia, vyakula vyenye mafuta mengi yanayozalishwa viwandani (iTFA) huhusisha vyakula vya kukaanga, na vitu vilivyookwa kama vile keki, biskuti na pai pamoja na milo iliyopakiwa au tayari. Vyakula hivi mara nyingi huwa na sukari nyingi, mafuta na chumvi nyingi.

Pia hupatikana katika nyama na bidhaa za maziwa ya ng'ombe, kondoo na mbuzi.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya vyakula vya aina hii kwa miaka ya karibuni, kutokana na unafuu wake wa bei, wataalamu wanasema.

Pia zina sifa kadhaa za kemikali na kimwili, kama vile kuwa dhabiti kwenye joto la kawaida na kuzifanya zifae kwa aina mbalimbali za bidhaa za chakula zilizochakatwa.

Uchaguzi wa mafuta na mafuta yanayotumiwa katika nchi nyingi huathiriwa na upatikanaji, gharama ya njia mbadala na uwezo wa sekta ya mafuta kufanya uvumbuzi.

Kulingana na Dkt Branca, kuna uwezekano kabisa wa kuviondoa kwenye mzunguko vyakula vya aina hii bila kuathiri uchumi na mahitaji ya watumiaji.

“Ni lazima kwa nchi kuweka vikomo. Kwa kusema kuwa hatutaki kuona mafuta na mafuta yoyote au vyakula vyenye zaidi ya asilimia moja ya lehemu au wanaweza hata kupiga marufuku kabisa kiungo. Kwa hivyo, kuna aina tofauti za kanuni lakini kwa hakika kanuni ambazo zitawataka wazalishaji kubadilisha kiungo.”

Hata hivyo, kanuni za namna hiyo ni lazima ziungwe mkono na kuwepo na ufuatiliaji wa kutosha ikiwa dunia inataka kufikia lengo, kwa mujibu wa Dkt Branca.

"Inawezekana kufanya hivi na tumetoa tuzo hivi karibuni kwa baadhi ya nchi kwa sababu zimeweza kuweka sera na kuzitekeleza. Kimsingi sasa watu wanaoishi katika nchi hizo hawatumii mafuta yanayotokana na bidhaa za viwandani na hivyo wanalindwa dhidi ya magonjwa ya moyo na mishipa.”

Januari 2024, WHO ilitunuku vyeti maalumu kwa nchi za Denmark, Lithuania, Poland, Saudi Arabia, na Thailand kama katika kutambua jitihada zao za kuondoa vyakula vya mafuta ya ziada.

Kwa sasa, nchi hizi ''zinaongoza duniani katika kufuatilia na kutekeleza sera zao za mafuta ya lehemu. Tunazihimiza nchi nyingine kufuata mwongozo wao,” mkurugenzi mkuu wa WHO alibainisha.

Hatua za Kimkakati

Mwaka 2018, WHO ilijiwekea malengo ya kuondoa vyakula vya iTFA kwenye mnyororo kwa kufukia mwaka 2023. Kushindwa kufikia lengo hili kutawaweka watu bilioni tano kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo na vifo.

“Tuliazimia kumaliza huu mkakati mwaka 2023,” Dkt Branca anasema.

Ili chakula kiwe na virutubisho, ni vyema kuwepo na matunda na mbogamboga. Picha: AA

Taisisi hiyo iliandaa mkakati ujulikanao kama REPLACE wenye kuwezesha serikali duniani kuja na sera zenye kulenga kuondoa vyakula vyenye mafuta ya ziada.

Ingawa utekelezwaji wa mkakati huo bado haujakamilika kwa kila nchi, Dkt Branca anasema kuna maendeleo ya kuridhisha katika mchakato huo.

Kwa mwaka 2023 pekee, sera mpya za utendaji bora zilianza kutumika katika nchi saba (Misri, Mexico, Moldova, Nigeria, Macedonia Kaskazini, Ufilipino, na Ukraine), afisa wa WHO anasema.

“Utakuwa ni mwenendo wa kidunia. Hata wazalishaji wa vyakula na mafuta wameelwa na kuukubali mchakato huu. Makampuni makubwa ya mafuta wamebadili bidhaa zao. Hili linawezekana tena kwa haraka sana,” Dkt Branca anaongeza.

"Uondoaji wa mafuta ya ziada unawezekana kiuchumi, kisiasa, na kiufundi na kuokoa maisha bila gharama yoyote kwa serikali au watumiaji," Dkt Tom Frieden, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Resolve to Save Lives alisema.

"Tunashuhudia ushindi katika vita hivi, lakini nchi ambazo hazina kanuni wala miongozo, ziko hatarini kuwa majalala ya bidhaa hizi zenye mafuta mengi. Kampuni za vyakula na mataifa zinawajibu wa kuhakikisha kuwa hili halitokei," aliongeza.

Upunguzaji matumizi ya mafuta

Wataalamu wanapendekeza matumzi ya mafuta kutoka kwenye mimea kama vile mahindi, alizeti, maharage ya soya, samaki wenye mafuta mengi, na mbegu kama vile kanola, mizeituni, karanga, na mafuta kutoka kwa karanga na parachichi.

Ingawa jukumu la msingi la kuwalinda raia kutokana na madhara ya mafuta yanayozalishwa viwandani ni la serikali, watu binafsi pia wanaweza kuchukua hatua za makusudi kupunguza ulaji wa mafuta ya ziada.

TRT Afrika