Chama kikuu cha upinzania nchini Tanzania (Chadema) kimefanya maandamano ya amani jijini Dar es Salaam kuitaka Serikali izingatie maoni ya wananchi katika marekebisho ya miswada mitatu iliyowasilishwa Bungeni.
Maandamano hayo, yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe na baadhi ya vinara kutoka Chadema akiwemo Tundu Lissu na Godbless Lema, yalipita kwenye mitaa tofauti ya jiji hilo yakiwa na jumbe tofauti, ukiwemo ule wa kupinga miswada ya uchaguzi iliyowasilishwa bungeni.
Chama hicho pia kimeitaka Serikali kushughulikia kile walichokiita hali ngumu ya maisha wanayopitia wananchi na kuishinikiza serikali kusikiliza maoni ya watu.
Ulinzi uliimarishwa katika kona zote za jiji la Dar es Salaam, kuepusha uvunjifu wa amani wakati wa maandamano hayo yaliyoanzia eneo la Buguruni kuelekea Ofisi za Umoja wa Mataifa.
Sauti za kama vile 'Tunataka Katiba Mpya,' 'Punguza Gharama za Maisha' ndizo zilitowala maandamano hayo ya kwanza kufanyika tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, mwaka 2021.
Baadhi ya miswada inayopigiwa kelele na Chadema ni ile ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa yote ya mwaka 2023.