Matokeo ya tetemeko la ardhi lenye nguvu Nchini Morocco / Picha: Reuters

Algeria imetuma salamu zake za rambirambi kwa nchi jirani ya Morocco kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililowaua zaidi ya watu 1000.

Kufikia Jumamosi alasiri idadi hiyo ilikadiriwa kufikia vifo 1,037 huku wengine wapitao 700 wakijeruhiwa kufuatia tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.0 lililotokea karibu na mji wa Marrakech, Ijumaa usiku kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi hiyo.

"Algeria inatuma rambirambi zake za kina na huruma ya dhati kwa familia za wahasiriwa wa ndugu zetu wa Morocco, na tunawatakia wote waliojeruhiwa, afueni ya haraka ," Wizara ya Mambo ya nje ya Algeria ilisema kwenye taarifa.

"Algeria inafuatilia kwa uchungu mkubwa, na huzuni, athari za tetemeko la ardhi lenye nguvu ambalo liligonga mikoa kadhaa Katika Ufalme wa Morocco," iliongeza.

Aidha, Algeria pia iliamua kufungua anga yake kwa ndege za kibinadamu na matibabu kuingia na kutoka Morocco kufuatia tetemeko la ardhi.

"Algeria iko tayari kabisa kutoa misaada ya kibinadamu na kuhamasisha nyenzo zote na rasilimali watu kwa mshikamano na watu wa kindugu wa Morocco iwapo watapokea ombi kutoka Ufalme wa Moroko," Urais Wa Algeria ulisema katika taarifa.

Shirika la Uchunguzi wa Jiolojia la Marekani (USGS) lilisema kuwa kitovu cha tetemeko hilo la ardhi, kilikuwa kilomita 75 (maili 46.6) kusini mashariki mwa Marrakech, kwa kina cha kilomita 18.5.

Vilevile, tetemeko pia lilihisiwa Katika nchi jirani za Algeria na Mauritania.

Mnamo 2004, zaidi ya watu 600 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 lilipotokea Kaskazini mashariki mwa Morocco.

TRT Afrika na mashirika ya habari