Jailosi anaamka kila asubuhi kufungua kibanda chake jijini Dar es Salaam, Tanzania, mtaa wa Kariokoo.
Yeye hutengeneza viatu, lakini sio viatu vya kawaida tu, viatu vya Masandale, kanda mbili au kobazi zinazoshonwa kutoka kwa tairi.
‘‘Hivi viatu ni maarufu sana mjini Arusha. Lakini vimesambaa sasa hadi maeneo mengine kama vile Iringa, Dodoma na Mbeya,’’ ameambia TRT Afrika.
Kwa kutumia kisu kikali, anachonga kipande cha tairi na kuanza kukipa umbo la kiatu. Amefanya kazi hii kwa miaka mingi, hana haja ya kufuata maagizo yoyote. Umahiri wake unaonekana anavyocheza na kisu mkononi.
‘‘Inanichukua kama dakika 15 au 20 kumaliza kiatu kimoja,’’ anaongeza.
Masandale ni maarufu sana kwa jamii ya Wamaasai wanao patikana sehemu za Kenya na Tanzania. Lakini kiatu hicho kimepokewa na kutumiwa pia na jamii nyingine kama vile Wakamba na Wakikuyu nhcini Kenya.
Kawaida, unaweza kutambua kiatu hicho kimetengenezewa jamii gani kwa kutazama mtindo au mshono wake.
Jailosi anasema alishangazwa sana kuona idadi ya tairi zinazoishia jalalani huku wengi hawajui cha kufanya nazo.
Ameambia TRT Afrika hapo aliona fursa ya kufanya biashara.
‘‘Watu wengi wanakuja kununua viatu hivi kwasababu vinadumu zaidi,’’ amesema. ‘‘ Yaani unaweza kutumia kwa muda mrefu sana.’’
Lakini mita chache tu kutoka kwa kibanda chake, Romani hutengeneza viatu sawa. Anasema ingawa anapata pesa, anaridhika zaidi
‘’Kila mahali unapoenda unaweza kuona milima ya matairi. Watu wanazitumia na kuzitupa. Hakuna mengi zaidi ya kufanya nayo. Kwa hivyo ni bora tutengenezee viatu kutoka.’’kuona matairi yanatumika vizuri.
Tanzania, kama nchi nyingine za Afrika inapambana na tatizo la usimamizi wa taka ya matairi.
Mnamo mwaka wa 2016, serikali ilianzisha sheria kali za kupiga marufuku uingizaji wa matairi yaliyotumika. Sheria hii pia inazuia uagizaji wa matairi na bidhaa za matairi zenye umri wa zaidi ya miaka 8.
Hii ilisababisha kupungua kwa utupaji wa matairi ya taka, lakini wachambuzi wanasema tatizo bado liko wazi sana.
Ellen Otaru ni mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Mazingira Tanzania, JET. Aliiambia TRT Afrika kuwa hakuna data ya kutosha kusaidia kupata suluhu zenye uhakika.
‘’Tunakosa utafiti na uchanganuzi sahihi juu ya utupaji wa matairi na una athari kamili kwa mazingira na maisha ya binadamu. Hakuna anayefuatilia kuona usimamizi wa udhibiti wa taka pia.’’
Imekuwa kawaida kuona milima ya matairi inayochomwa. Moshi mweusi unaotoka hutoa gesi zenye sumu kwenye angahewa.
Matairi yanajulikana kuwa hayaozi kwani yanaweza kudumu kwa muda mrefu kwenye madampo. Ingawa utafiti zaidi unahitaji kufanywa, wataalam wanaamini hata wanapokaa hutoa sumu ambayo ni hatari.
Hivi sasa, zaidi ya matairi bilioni moja hufikia mwisho wa maisha yao muhimu kila mwaka. Lakini badala ya kutafuta suluhu endelevu, nchi nyingi zilizoendelea, hupeleka tatizo hilo kwa mataifa mengine.
‘’Katika baadhi ya nchi zilizoendelea, kama Kanada, wanachakata matairi taka ili kutengeneza mafuta, lakini katika Afrika hatuwezi kufanya hivyo bado kwa sababu ina gharama kubwa sana,’’ anasema Ellen Otaru.
‘’Nchi nyingine zinasafirisha kwa urahisi matairi yao yaliyotumika kwa nchi zinazoendelea, lakini hakuna anayefuatilia kujua jinsi yanavyotumika,’’ anaongeza.
Barani Afrika, matairi mengi yaliyotumika huishia kuchomwa moto. Wataalamu wa afya wanaonya dhidi ya hili kwani hutoa gesi hatari kwenye angahewa ikiwa ni pamoja na sianidi, monoksidi kaboni na dioksidi sulfuri.
Lakini watu wengi zaidi wanakuja na njia bunifu za kutumia tena taka hizi za mpira ambazo zimekuwa donda ndugu, wakati mwingine zinatumika kwa urembo na kuhifadhi maeneo.
‘’Kuna vijana wengi huko nje wanafanya vizuri katika kuchakata matairi ya zamani kwa ajili ya mimea na bustani, viatu na ujenzi wa vyoo.’’ Anasema Ellen. ‘’ Lakini juhudi hizi zinahitaji kupanuliwa katika ngazi za serikali au hata za bara ili kuleta athari kubwa zaidi.’’
Utafiti unapoendelea kuhusu ni ipi njia bora ya kushughulikia taka za tairi zilizotumika, au bora zaidi, kutafuta chaguo mbadala bora endelevu wa matairi, Jailosi na Romani wataendelea kutoa mchango wao mdogo katika kuhifadhi mazingira kiatu kwa kiatu.