Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva./Picha: @jumuiya

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kuandaa rasimu ya katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya hiyo wakati wa mkutano wao wa Novemba 30, 2024.

Mkutano huo wa 24 wa wakuu wa nchi za EAC pia, unafanyika wakati Jumuiya hiyo ikitimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, uundwaji wa rasimu hiyo ni maelekezo kutoka kwenye mkutano wa awali wa wakuu wa nchi za EAC.

“Kamati yetu imekamilisha ukusanyaji maoni kutoka baadhi ya nchi wanachama, tunategemea tuwe tumekalisha zoezi hilo ifikapo Juni 30, 2025,” alisema Nduva.

Wakuu wa nchi hizo pia wanatarajiwa kujadiliana changamoto na fursa mbalimbali za Jumuiya hiyo, wakati ikiadhimisha miaka 25.

Hadi kufikia Septemba 2022, Jumuiya ya EAC ambayo inaundwa na nchi wanachama 8, imeongeza mwenendo wa biashara baina yao, kutoka Dola Bilioni 7.1 mwaka 2019 hadi kufikia Dola Bilioni 10.17 Septemba 2022, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ni muundo wa muundo wa kisiasa unaounganisha nchi nane ambazo ni Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda

TRT Afrika