kenya bnb security

Mamlaka ya udhibiti wa usalama binafsi PSRA nchini Kenya imewaagiza wafanya biashara wa kukodi vyumba vya muda Air BnB, kushikilia vitambulisho rasmi vya wateja wao wanapokodi vyumba n akuchukua maelezo yote kuwahusu kw alengo la kuimarisha usalama.

Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Usalama Binafsi, Fazul Mahamed alisema maagizo hayo yanalenga kudhibiti matukio ya ukosefu wa usalama katika taasisi hizo kufuatia mfululizo wa mauaji ya kutisha tangu mwaka uanze.

Chini ya agizo hilo wamiliko wa vyumba watatakiwa kurekodi muda wa kuingia au kutoka kwa kila mtu binafsi pamoja na magari au pikipiki zinazoingia au kutoka kwenye vituo hivyo.

Vutambulisho na vyeti vingine vyovyote vitarejeshwa kwa wateja punde wanapoondoka.

Taarifa hiyo inanukuu kifungu cha sheria cha 48, ambacho kinampa mamlaka afisa usalama wa kibinafsi aliyepo kwenye eneo la kuingilia eneo au mali yoyote kumtaka mtu kujitambulisha, kusajili muda wa kuingia na kutoka kwa mtu huyo na kuhifadhi kwa muda hati za utambulisho wa mtu huyo.

Usalama wa data za wateja

''Taasisi zote pia zitahitajika kudumisha daftari la matukio ya usalama ili kurekodi matukio muhimu ya kila siku yanayohusiana na usalama wa wakaazi ndani ya majengo na kuhakikisha CCTV na kamera za usalama ziko katika hali ifaayo ya kufanya kazi,'' iliendelea kusema taarifa hiyo.

Hata hivyo Mamlaka hiyo ilitoa onyo kali kwa wafanya biashara hao kutofuja au kutumia vibaya maelezo binafsi ya wateja wao.

''Mtoa huduma za usalama wa kibinafsi ambaye anakiuka Kifungu cha 48 cha Sheria hiyo, hutumia hati/maelezo ya kitambulisho yaliyotolewa na watu binafsi wakati wa kuingia kwa eneo au mali yoyote kwa madhumuni mengine isipokuwa kwa ajili ya utambulisho, na/au kwa makusudi kushindwa kutii agizo hili, anavunja sheria,'' Taarifa ilisema.

Kwa mujibu wa onyo hilo, watakaokiuka sheria hiyo pamoja na kufutwa kwa leseni, atawajibika kwa adhabu iliyowekwa chini ya sheria ya kulinda maelezo ya siri ya watu, au sheria nyingine yoyote ambayo ni kubwa zaidi.

katika siku chache zilizopita, wanawake kadhaa wamekutwa wameuawa katika vyumba vya BnB jijini Nairobi ambapo mmoja alikutwa amechomwa kisu na mwingine, katika tukio iliyohusiana, alikutwa amekatwa katwa viungo vyake kwa kinachoaminiwa huenda ilikuwa tambiko la kishirikina.

Washukiwa kadhaa wanazuiliwa kusaidia polisi na uchunguzi.

TRT Afrika