Viongozi wa bara la Afrika wanadai kuwa mfumo wa sasa wa kifedha duniani hautaweza kutoa usaidizi unaohitajika ili kufikia ajenda kabambe na ya kuleta mabadiliko ya Afrika.
Marais na viongozi wa tabaka mbali mbali barani wamekutana jijini Nairobi, nchini Kenya katika mkutano wa kila mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika yaani Africa Development Bank, AfDB.
"Tunauliza AfDB kusaidia mfumo wa mikopo wa Kiafrika ambao utasaidia kuweka taarifa za kweli katika usanifu wa kifedha ili thamani ya Afrika iweze kuonekana wazi," Rais William Ruto aliuambia mkutano huo.
Viongozi wamefanya majadiliano kuhusu mabadiliko ya Afrika, na marekebisho ya Usanifu wa Fedha Ulimwenguni.
"Tunahitaji mfumo wa kifedha ambao una ufadhili wa muda mrefu, viwango vya chini vya riba, ikijumuisha ruzuku. Tunahitaji pia ufadhili kwa kiwango na ambao unazingatia madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwetu ili kama kuna majanga, mfumo huo wa fedha inasaidia," Rais Ruto ameongezea.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika amesema bara linaelewa mahitaji yake kutoka kwa jamii ya kimataifa.
"Tuna vipaumbele. Tumefafanua wazi mipango na tunazungumza na jumuiya ya kimataifa, si kwa ajili ya misaada, tunaomba tuchukuliwe kwa usawa." Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Tume ya AU amesema.
"Hapa barani Afrika, michango ya ufadhili wa nje katika maendeleo ya Afrika imekuwa chini ya matarajio, na kutafsiri kwa kweli kuwa ukosefu wa haki kwa Afrika," Faki ameongezea.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt. Akinwumi Adesina anasema dunia inabadilika na Afrika inahitaji kuwa katika majadiliano ya kuamua jinsi fedha za maendeleo zinavyofaa kugawanywa.
"Usanifu wa kifedha wa kimataifa hauangazii masuala ya Afrika wala kuwasilisha kwa Afrika. Sauti yetu inapaswa kuwa kwenye meza. Usanifu wa kifedha wa kimataifa unahitaji kuunda usawa, haki, uwakilishi na ushirikishwaji," Dkt. Adesina amesema.
Rais wa Rwanda Paul Kagame naye amehimiza kuwa usambazaji wa rasilimilami duniani si kwa njia ya kunufaisha Afrika.
"Kuna rasilimali nyingi katika ulimwengu huu, lakini zinasambazwa bila usawa. Je, tunabadilishaje usanifu wa sasa wa kifedha kama tulivyo nao, ili ujumuishe kwa kiasi kikubwa na kwa kuonekana masilahi ya bara letu? " Rais Kagame ameuliza.
"Katika miongo michache, mahali pekee katika ulimwengu huu patakuwa na tabaka la kati linalokua ni Afrika. Kwa hivyo, ni kwa faida ya ulimwengu wote ambao umeiweka Afrika pembeni kuchangia ustawi wa bara letu. Kwa sababu ukuaji wa Afrika, kulingana na tabaka hili la kati, unachangia ukuaji wa ulimwengu wote," Rais Kagame ameongezea.
Naye rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amehimiza viongozi wenzake kutimiza maamuzi ya mabadiliko ya mfumo wa fedha wa kimataifa.
"Ikiwa sote tutashirikiana kama bara, ninaamini kasi yetu ya maendeleo na kisasa itakuwa ya haraka zaidi. Lakini tukiendelea kuendeleza nchi zetu katika maghala, itachukua muda mrefu zaidi," amesema Rais Mnangagwa.
Rais wa AfDB Adesina alikaribisha uamuzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, la kuunda kiti cha tatu cha Afrika katika Bodi yake, na kujumuishwa kwa Afrika Kusini na Umoja wa Afrika katika muungano wa nchi za G20, akiongeza kuwa alifikiri kunapaswa kuwa na kiti cha pili cha Nigeria katika G20.