Sekta ya usafiri wa ndege inaangalia mapato ya takriban dola trilioni moja mwaka huu 2024. Hata hivyo, gharama pia zitakuwa kwenye rekodi ya juu ya $936 bilioni.
"Faida halisi itakuwa $30.5 bilioni. Hiyo si rekodi kwa bahati mbaya, na inawakilisha kiasi halisi cha zaidi ya 3%. Lakini ukizingatia pale tulipokuwa miaka michache tu iliyopita, ni mafanikio makubwa," Mkurugenzi Mkuu wa IATA, Willie Walsh, aliuambia mkutano mkuu wa 80 wa Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA) mjini Dubai.
"Mashirika ya ndege yataunganisha karibu watu bilioni tano zaidi ya njia 22,000 kwenye safari milioni 39. Na tutawasilisha tani milioni 62 za shehena—ikiwezekana $8.3 trilioni katika biashara," Welsh ameongezea.
Afrika bado inajikakamua
Biashara ya sekta ya usafiri wa ndege bado ipo chini barani Afrika.
Afrika inachukua asilimia 3 pekee za anga duniani.
Hata hivyo, IATA inatabiri kuwa mataifa saba kati ya 10 ya juu ya uchumi wa anga yanayokuwa kwa kasi zaidi katika miaka 20 ijayo yatakuwa barani Afrika.
Chama cha Wafanyabiashara wa Anga barani Afrika (AfBAA) kinasema kuna biashara kubwa ya ukodishaji wa ndege barani Afrika.
Ikiwa na ndege 418 za biashara, Afrika Kusini ina ndege nyingi binafsi za biashara barani, ikifuatiwa na Kenya yenye ndege 137 na Nigeria 109.
"Afrika inatoa fursa za kuvutia za uwekezaji kwa wafanyabiashara wa anga za kimataifa kutokana na kuongezeka kwa tabaka lake la kati, uchumi tajiri wa rasilimali, na uwezekano wa soko la usafiri wa anga ambao haujatumika," alisema Gavin Kiggen, makamu mwenyekiti wa AfBAA.
Safari za ndege za kibiashara zinaendeshwa kati ya Afrika Magharibi na Ulaya, Afrika Kaskazini hadi Ulaya, na Afrika Mashariki hadi Mashariki ya Kati. Lakini bado, safari nyingi za ndege za biashara zinaendeshwa katika njia za ndani ya Afrika.
"Kuna mahitaji yanayoongezeka ya huduma za kukodisha ndege, vituo vya matengenezo, na mauzo ya ndege katika eneo hilo," Kiggen ameongezea.
Kulingana na Kiggen, serikali za Afrika na wadhibiti wanaanza kuelewa kwamba urubani wa ndege za biashara ni chombo cha thamani cha biashara, ambacho kimesababisha uwekezaji uliorahisishwa katika bara.
“Uelewa wa thamani ya usafiri wa anga kwa Afrika unafungamana na hitaji la mashirika kusafiri ili kujitanua na kuwa na mafanikio ya kibiashara, iwe ndani au nje ya nchi. Hii ndiyo sababu makampuni kama wanachama wa AfBAA wanaimarisha kila mara nyayo zao,” Kiggen alisema.
Changamoto ya usafiri wa ndege Afrika
Ukosefu wa maelezo , kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, migogoro ya silaha, miundombinu duni ya viwanja vya ndege, mchakato mrefu wa kibali cha ndege, na ada kubwa za kutua na kushughulikia ardhi ni miongoni mwa orodha ndefu ya changamoto zinazoathiri shughuli za usafiri wa anga barani Afrika.
wataalma wanasema pia ushuru mwingi na ada za uwanja wa ndege ni kikwazo kingine. Kulingana na IATA, Afrika ina baadhi ya kodi na tozo za juu zaidi zinazotozwa kwa mafuta ya anga na ada za juu zaidi za kutua.
Gharama hizi hupitishwa kwa abiria, kuweka nauli za ndege juu na kufanya safari za ndege kuwa ghali zaidi kuliko sehemu nyengine ulimwenguni.