Ugonjwa wa Marburg huenezwa kupitia Popo wa matunda aina ya rousette./Picha: Getty    

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa wito wa ushirikiano wa pamoja kati ya nchi wananchama wa jumuiya hiyo katika kupambana mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.

Tayari, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonesha wasiwasi juu ya ya kusambaa wa ugonjwa huo kwenye mipaka ya Rwanda na nchi za DRC, Uganda, and Tanzania.

“Kuna haja kubwa ya nchi wanachama wa EAC kushirikiana pamoja ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huu, kupitia uimarishaji wa shughuli za upimaji kwenye mipaka yetu,” alisema Andrea Aguer Ariik Malueth, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Miundombinu na Mambo ya Kijamii.

Wito huo unakuja wakati Rwanda imeanza kupima wasafiri wote wanaoingia nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali.

Katibu Mkuu huyo, pia ametoa rai ya kuongeza uelewa na hamasa za kupambana na ugonjwa huo unaosababisha vifo.

Vimelea vya ugonjwa wa Marburg./Picha: Getty

Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt, Ujerumani na Belgrade huko Serbia.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.

TRT Afrika