Afrika Kusini inasema kesi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israeli inaongeza juhudi za kimataifa kuhakikisha amani katika Mashariki ya Kati. /Picha: Reuters

Kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israeli katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) itaendelea na Afrika Kusini itawasilisha file ya ukumbusho mwezi ujao, ofisi ya rais ilisema katika taarifa yake Jumanne.

"Afrika Kusini inakusudia kutoa ukweli na ushahidi kuthibitisha kuwa Israeli inatekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari huko Palestina," ilisema taarifa hiyo.

"Kesi hii itaendelea hadi mahakama itakapotoa uamuzi. Wakati kesi hiyo ikiendelea, tunatumai Israeli itatii amri za muda za mahakama zilizotolewa hadi sasa."

Matamshi hayo yanajiri huku kukiwa na ripoti kwamba wanadiplomasia wa Israeli wanaagizwa kuwashawishi wajumbe wa Bunge la Marekani kuishinikiza Afrika Kusini kufuta kesi hiyo.

Amani katika Mashariki ya Kati

Afrika Kusini ilisema kesi yake ya mauaji ya halaiki dhidi ya Israel inawakilisha juhudi zinazoongezeka za kimataifa kuelekea kuhakikisha amani katika Mashariki ya Kati.

Nchi kadhaa, zilijiunga kwenye kesi, ambazo ni Uturuki, Nicaragua, Palestina, Uhispania, Mexico, Libya na Colombia, zote zimejiunga na kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mbele ya umma mnamo Januari.

Afrika Kusini iliwasilisha kesi hiyo katika mahakama hiyo iliyoko "The Hague" mwishoni mwa 2023, ikiishutumu Israeli, ambayo imeshambulia kwa bomu Gaza tangu Oktoba mwaka jana, kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya 1948.

Mwezi Mei, mahakama kuu iliiamuru Israeli kusitisha mashambulizi yake katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah.

Ilikuwa ni mara ya tatu kwa jopo la majaji 15 kutoa maagizo ya awali ya kutaka kudhibiti idadi ya vifo na kupunguza mateso ya kibinadamu katika eneo lililozingirwa, ambapo idadi ya majeruhi imevuka 40,000.

TRT Afrika