Felix Koskei, mkuu wa wafanyakazi wa serikali ya Kenya na mkuu wa utumishi wa umma, ameagiza kusimamishwa kazi kwa maafisa wakuu sita na maafisa 67 wa polisi kwa tuhuma za ufisadi.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed siku ya Alhamisi, Koskei alisema maafisa waliosimamishwa kazi walijihusisha na "ufisadi na ukiukwaji wa sheria za ununuzi ndani ya taasisi zao."
Pia aliyesimamishwa kazi ni Esther Wanjiru Chege, mhasibu katika Mamlaka ya Barabara za Vijijini Kenya (KeRRA), kwa "madai ya mgongano wa kimaslahi na umiliki wa mali isiyoelezeka."
Koskei alisema watu walioathiriwa wanachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ambayo ilipendekeza kusimamishwa kwao.
Wakurugenzi wakuu waliomba kuondoka
Fredrick Mwati, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Maendeleo ya Tanathi Water Works, ambaye alisimamishwa kazi Jumatano, "anachunguzwa kwa makosa ya ununuzi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Mradi wa Usambazaji Maji wa Hifadhi ya Viwanda ya Ngozi."
Stephen Ogenga, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Viwanda (NITA), alisimamishwa kazi kwa "madai ya ukiukwaji wa sheria katika utoaji wa zabuni ya vifaa katika NITA."
Stanvas Ong’alo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, amesimamishwa kazi kutokana na "madai ya ubadhirifu wa KSh490 milioni (dola milioni 3.22) kupitia malipo yasiyo ya kawaida."
Benjamin Kai Chilumo, Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Huduma Center, ameagizwa kujiuzulu kuhusu "madai ya ufisadi alipokuwa akihudumu katika Serikali ya Kaunti ya (pwani) ya Kilifi kama Afisa Mkuu wa Fedha."
Amejitolea 'kutokomeza rushwa'
Peter Gitaa Koria, Mkurugenzi Mtendaji wa kivutio cha utalii cha Bomas of Kenya, amesimamishwa kazi kwa "madai ya ukiukwaji wa taratibu za ununuzi wa vifaa vya taasisi hiyo."
Anthony Wamukota, Meneja Mkuu wa Usanifu na Ujenzi katika Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya (KETRACO), amesimamishwa kazi kutokana na "madai ya ukiukwaji wa sheria kuhusiana na kandarasi ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa 400KV Loiyangalani."
“Aidha, EACC imemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kuwasimamisha kazi maafisa 67 wa polisi wanaohusishwa na ufisadi,” Mohamed alisema kwenye taarifa hiyo.
"Serikali inasalia imara katika dhamira yake ya kutokomeza ufisadi ambao, yeye (Koskei) anashikilia, unadhoofisha ajenda yake ya maendeleo," Mohamed aliongeza.