Mamlaka zinahusisha matukio ya mara kwa mara ya migodi ya dhahabu kwa kupuuza itifaki za usalama. / Picha: AA

Watu saba walifariki baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka katika Kaunti ya Siaya Magharibi mwa Kenya siku ya Jumanne, polisi walisema.

Tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Lumba, takriban kilomita 400 (kama maili 250) kutoka mji mkuu wa Nairobi.

Mkuu wa polisi wa Siaya Kleti Kimaiyo alithibitisha vifo hivyo kwa Anadolu. "Naweza kuthibitisha watu saba wamepoteza maisha katika tukio hili la kusikitisha. Wengine saba waliokolewa na timu ya wenyeji ambao walikuwa wahudumu wa kwanza pamoja na vikosi vya uokoaji," alisema.

Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Bondo.

Itifaki za usalama

Ben Bera, afisa madini wa kikanda wa eneo la Siaya, alihusisha kuporomoka kwa mgodi mara kwa mara katika kanda hiyo na wachimbaji wadogo wa madini kutozingatia itifaki za usalama.

"Wachimbaji wengi wa madini hawafuati miongozo muhimu ya usalama, ambayo inasababisha ajali hizi mbaya. Ni lazima tutekeleze kanuni kali ili kuhakikisha usalama wa wachimbaji wetu," aliiambia Anadolu.

Katika kisa sawia mnamo mwezi wa Mei, mgodi usio rasmi wa dhahabu uliporomoka katika kaunti ya Marsabit, na kusababisha vifo vya wachimba migodi watano.

TRT Afrika