Takriban watu 30 wamekufa maji na 167 hawajulikani walipo baada ya mashua kupinduka kwenye mto Congo jioni ya Ijumaa kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waziri wa jimbo aliambia Reuters siku ya Jumapili.
Didier Mbula, waziri wa afya wa mkoa wa Equateur, alisema kuwa watu 189 wameokolewa na kwamba msako bado unaendelea.
“Kwa mujibu wa idadi tuliyonayo hadi sasa katika Serikali ya Mkoa, maiti 30 zimeopolewa, 167 hazijapatikana,” alisema Mbula.
Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika mto Congo, ambapo maboti mara nyingi hupakiwa zaidi ya uwezo wao.
Kupakia kupita kiasi
Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na kusafiri kwa mto ni jambo la kawaida.
Boti iliyotengenezwa kienyeji ambayo ilipinduka karibu na mji wa Mbandaka ilikuwa imejaa kupita kiasi, ikiwa imebeba zaidi ya watu 300, na ilikuwa ikisafiri usiku, Mbula alisema.
"Tunafikiri kwamba idadi ya watu inaweza kupanda kwa sababu tumepata maiti 30 pekee," alisema.