Serikali ya DRC bado inapambana dhidi ya vuguvugu la kikundi cha waasi cha M23\ PICHA: AP Maktaba.

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Watu 20 wameuawa nchini Burundi katika shambulio la watu wenye silaha kwenye eneo la mpakani mwa Burundi na DRC. Kundi la waasi wa RED Tabara wamedai kuwa wamehusika na shambulio hilo.

Watu 20 wameuwawa na wengine 9 kujeruhiwa katika shambulio la watu wenye silaha katika kijiji cha Vugizo eneo la Gatumba mpakani mwa Burundi na DRC, ikiwa ni kwenye umbali wa kilomita 30 na mji Bujumbura.

Taarifa rasmi ya serikali imethibitisha kuwa shambulio la kikatili lilifanyika siku ya Ijumaa saa mbili usiku katika kijiji cha Vugizo dhidi ya makaazi 9 ya watu na kuwalenga watu wasio na hatia wakiwemo watoto na wanawake.

''Watu 20 wameuawa kikatili wakiwemo watoto 12 wa chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wanawake watatu wakiwemo wawili wajawazito,'' alitangaza Katibu Mkuu na Msemaji wa Serikali Jérôme Niyonzima katika tamko rasmi.

Aidha katika shambulio hilo pia ''wameuawa wanaume watano akiwemo polisi mmoja aliyekwenda kujaribu kuwanusuru raia hao,'' alisema Niyonzima

Serikali ya Burundi imejizuia hadi sasa kutaja kikundi kilichohusika na shambulio hilo. Inasema uchunguzi umeanzishwa kujua ni kina nani walihusika katika shambulio hilo ''Tutafanya kila juhudi kuwagundua waliohusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria, '' aliongeza kusema Msemaji wa Serikali Jérôme Niyonzima.

Wajumbe wa Serikali ya Burundi walikuwa katika eneo la tukio mapema Ijumamosi hii kuwafariji raia wa maeneo hayo na kuchukua dhamana ya matibabu kwa waliojeruhiwa.

Hata hivyo, waasi wa Burundi wa RED Tabara wamedai kwamba wamehusika katika shambulio hilo lakini kwenye taarifa yao mitandaoni wanasema walilenga vituo vya jeshi na polisi katika eneo hilo la mpakani la Gatumba.

''Wapiganaji wetu walioko Burundi walishambulia kituo cha mpakani cha Vugizo eneo la Gatumba. Askari tisa na polisi mmoja waliuawa. Tulihodhi pia silaha moja ya FM Kalash na mbili za Ak-47 pamoja na zana nyingi.''

Imekuwa vigumu kuthibitisha taarifa hizo za kikundi cha Red Tabara.

Waasi hao ambao wamedaiwa kuweka ngome yao Mashariki mwa DRC wamekuwa wanashinikiza mazungumzo na Serikali ya Burundi lakini Serikali imekuwa ikisema kuwa haiwezi kuzungumza na waasi hao.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alisema hivi karibuni kwamba Serikali yake iko tayari kuwapokea waasi kama raia wa Burundi iwapo watajisalimisha na kujiunga na juhudi za ujenzi wa taifa.

Serikali ya Burundi ilipeleka majeshi yake Mashariki mwa DRC katika mpango wa kukabiliana na makundi ya waasi wa Burundi kikiwemo kikundi cha Red Tabara.

TRT Afrika