Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa kwa sasa ndiyo kituo pekee cha matibabu kinachofanya kazi katikati mwa Gaza / Picha: AA

Huku mamia ya wagonjwa wakisubiri msaada, Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa inatatizika kutoa huduma za matibabu kwa wahasiriwa wa shambulio baya la Israeli katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza.

Takriban watu 274 waliuawa na wengine karibu 700 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la Israeli katika kambi hiyo siku ya Jumamosi, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo.

Mamia ya waathiriwa wameachwa wakiwa wamelala juu ya sakafu ya hospitali huku madaktari wakikimbia kutoa huduma ya matibabu licha ya kuwa na uhaba wa vifaa vya matibabu.

"Idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wanaofika hospitalini inazidi uwezo wa hospitali hio," Ismail al Thawabta, mkurugenzi wa Ofisi ya Chombo cha Habari ya Serikali ya Gaza, aliiambia Anadolu siku ya Jumapili.

"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kuingilia kati na kusaidia hospitali kwa kutoa vifaa vya matibabu na jenereta za umeme ili kuhakikisha utoaji wa huduma bila kukatizwa," alisema.

Siku ya Jumatano, hospitali hiyo ilisema kwamba moja ya jenereta zake mbili ilikuwa imesimama kwa sababu ya ukosefu wa mafuta.

Janga la kibinadamu

Matukio haya yanaashiria uwezekano wa kuokea kwa "janga la kibinadamu" ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa wengi wa Kipalestina na watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati, ilionya.

"Hali katika Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa ni mbaya na ya hatari sana. Tunataka kusitishwa mara moja kwa vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya raia,” Thawabta alisema.

Afisa huyo wa Palestina alisema kuwa mashambulizi ya Israeli yamesitisha shughuli za hospitali 33 kati ya 35 za Gaza, na kusababisha "mgogoro wa kibinadamu."

Hospitali ya Mashahidi wa Al Aqsa na Hospitali ya Ulaya ndio vituo viwili pekee vya matibabu vinavyoendeshwa na serikali ambavyo bado vinafanya kazi huko Gaza, kulingana na ofisi ya vyombo vya habari.

Kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo, zaidi ya Wapalestina 36,800 wameuawa huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na zaidi ya 83,500 kujeruhiwa.

Miezi minane baada ya vita vya Israeli, maeneo makubwa ya Gaza yamegeuzwa kuwa magofu huku kukiwa na kizuizi cha uingizaji wa chakula, maji safi na dawa.

TRT World