Ndege za Israel zimeshambulia Gaza kujibu roketi kutoka eneo la Palestina baada ya polisi wa Israel kuvamia eneo la Msikiti wa Al Aqsa usiku kucha.
Redio ya Hamas iliripoti kuwa mashambulizi ya Israel mapema siku ya Jumatano yaligonga shabaha kadhaa ndani ya mji wa Gaza na katika kambi ya wakimbizi.
Hakukuwa na ripoti ya mara moja juu ya majeruhi huko Gaza.
Mashambulizi hayo ya angani yametokea baada ya wanajeshi wa Israel kuvamia eneo la tatu takatifu kwa Waislamu huko Jerusalem Mashariki panapokaliwa kwa mabavu, kwa kutumia mabomu ya gesi na guruneti huku Wapalestina wakisali katika wiki ya pili ya Ramadhani.
Mashahidi na Hilali Nyekundu ya Palestina pia waliripoti kwamba wanajeshi wa Israeli wamewapiga waumini, na kuwaacha wengi wamejeruhiwa, na kuzua hofu ya mvutano mkubwa.
Baadaye, Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilisema Wapalestina 12 walijeruhiwa kutokana na risasi za mpira na kupigwa. Iimeongeza kuwa vikosi vya Israel vinawazuia madaktari wake kufika eneo hilo.
Picha za video zilionyesha wanawake na watoto wakipiga mayowe kuomba msaada wakati wanajeshi wa Israel wakifanya mashambulizi.
"Nilikuwa nimekaa kwenye kiti nikisoma [Quran]," mwanamke mzee aliambia shirika la habari la Reuters nje ya msikiti, akijitahidi kuvuta pumzi. "Walirusha mabomu ya kustaajabisha, moja likapiga kifua changu," alisema huku akianza kulia.
Waumini hao wanasema wakilazimika kuondoka msikitini. Wanajeshi wa Israel pia walivunja madirisha ya sehemu ya kusini ya msikiti huo, walioshuhudia waliongeza.
Polisi ya Israel imesema katika taarifa yake imewakamata makumi ya Wapalestina waliokuwapo msikitini, sehemu ya utamaduni wa dini ambayo Waislamu hukaa msikitini humo usiku kucha kuswali na kusoma Qur'ani Tukufu.
Wakili wa Palestina Firas al Jibrini alisema polisi walikamata karibu watu 500 ambao walichukuliwa kuhojiwa
Ghasia za Israel katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu zilizusha maandamano kutoka kwa Wapalestina.