Khader Adnan

Mpalestina Khader Adnan ambaye alikuwa mshirika wa kundi la Islamic Jihad la Palestina amefariki dunia katika jela ya Israel baada ya mgomo wa kula kwa siku 87.

Mamlaka ya magereza ya Israel ilisema Adnan, anayeshutumiwa na Tel Aviv kwa mashtaka ya ugaidi, alihamishwa hadi hospitali baada ya kushindwa kwa majaribio ya kumzindua na alitangazwa kufariki mapema Jumanne.

Israel ilisema Adnan "alikataa kufanyiwa vipimo vya afya na kupokea matibabu" na "alipatikana akiwa amepoteza fahamu kwenye seli yake" mapema asubuhi.

Wakili wa Adnan aliishutumu Israel kwa uzembe wa kiafya.

"Baada ya siku 36 za kukamatwa kwa Adnan, tulidai ahamishwe katika hospitali ya kiraia ambapo anaweza kufuatiliwa ipasavyo.

Kwa bahati mbaya, ombi kama hilo lilitimizwa kwa ukaidi na kukataliwa na wakuu wa magereza wa Israel,” wakili Jamil Al Khatib alisema.

"Khader Adnan ameuawa kwa damu baridi," Chama cha Wafungwa wa WAED huko Gaza kiliiambia Reuters kujibu.

Roketi zilizo rushwa kutoka Gaza

Muda mfupi baada ya kifo cha Adnan kutangazwa, ving'ora vilisikika katika jumuiya za mpakani mwa Israel na Gaza, na kuwatuma wakaazi kukimbilia hifadhi.

Jeshi la Israel limesema roketi tatu zilirushwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea eneo la Israel, lakini zikaanguka katika maeneo ya wazi.

"Mapambano yetu yanaendelea na adui atatambua kwa mara nyingine tena kwamba uhalifu wake hautapita bila majibu. Upinzani utaendelea kwa nguvu zote na dhamira,” ilisema taarifa ya Palestina Islamic Jihad.

Adnan, mwenye umri wa miaka 45, anayetoka katika jiji linalo kaliwa kwa mabavu la Jenin, alikuwa mtu maarufu wa Jihad katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ambao ulitekwa na Israel katika vita vya 1967.

Kwa mujibu wa Chama cha Wafungwa wa Kipalestina, Adnan alikuwa amezuiliwa na Israel mara 12, akitumia takriban miaka minane jela, hasa chini ya kizuizi cha utawala.

Israel ilimshutumu Adnan kwa kuunga mkono ugaidi, kujihusisha na kundi la kigaidi na uchochezi. Alifanya takriban migomo mitano ya kula katika nyakati tofauti alizokuwa kizuizini tangu 2004.

Reuters