Jeshi la Israel limesema "limemuua" kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah katika shambulio la anga kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut, ingawa kundi hilo bado halijatoa maoni yoyote kuhusu hatima yake.
''Vikosi vya Israel vimemuua mkuu wa Hezbollah ya Lebanon Sayyed Hassan Nasrallah,'' msemaji wa jeshi anayezungumza Kiarabu Avichay Adraee alisema, siku moja baada ya shambulio la Israel katika viunga vya kusini mwa Beirut.
"Hassan Nasrallah amekufa," msemaji wa jeshi Luteni Kanali Nadav Shoshani alitangaza kwenye X. Msemaji wa Jeshi Kapteni David Avraham pia alithibitisha kwa AFP kwamba mkuu wa Hezbollah "ameuawa " kufuatia shambulio la Ijumaa kwenye mji mkuu wa Lebanon.
Iwapo itathibitishwa, kifo cha Nasrallah kitaleta pigo kubwa kwa kundi la Lebanon ambalo ameongoza tangu 1992.
Mawasiliano na Nasrallah 'yametoweka ' tangu Ijumaa usiku
Chanzo karibu na kundi la Hezbollah la Lebanon kilisema mawasiliano ya Jumamosi yamepotea tangu jana jioni na chifu Hassan Nasrallah, baada ya Israel kusema "imemuua" katika shambulio kwenye ngome ya kundi hilo la Beirut kusini mwa kundi hilo.
“Mawasiliano na Sayyed Hassan Nasrallah yamepotea tangu Ijumaa jioni,” kilisema chanzo hicho kikiomba hifadhi ya jina ili kuzungumzia mambo nyeti. Hakuthibitisha kama Nasrallah aliuawa.
Milipuko iliyotokea kusini mwa Beirut Ijumaa ndiyo mikali zaidi kukumba ngome ya kundi hilo tangu Israel na Hezbollah zilipoingia vitani mara ya mwisho mwaka 2006.
Hassan Nasrallah ni nani?
Hassan Nasrallah alizaliwa mnamo Agosti 31, 1960, katika kijiji cha Bazouriyeh, karibu na Tiro kusini mwa Lebanon.
Amemuoa Fatima Yassin, na wana watoto watano: Hadi, Zeinab, Mohammad Jawad, Mohammad Mahdi, na Mohammad Ali.
Mwanaye mkubwa, Hadi, aliuawa katika mapigano na jeshi la Israel kusini mwa Lebanon mwaka 1997.
Nasrallah alipata elimu ya kidini katika chuo cha kidini cha Waislamu wa Shia huko Lebanon, Iraqi na Iran. Alijiunga na vuguvugu la kisiasa la Amal katika shule ya upili na akapanda ofisi yake ya kisiasa mnamo 1979.
Mwaka 1982, huku kukiwa na kutoelewana juu ya jinsi ya kupinga uvamizi wa Israel dhidi ya Lebanon, Nasrallah na wengine waliondoka Amal na kujiunga na Hezbollah, kundi jipya lililoanzishwa. Alipewa jukumu la kuhamasisha wapiganaji katika Bonde la Bekaa nchini humo.
Kufikia 1985, Nasrallah alihamia mji mkuu Beirut na kuwa naibu mkuu wa eneo hilo. Baadaye, alichukua jukumu la mtendaji mkuu, aliyepewa jukumu la kutekeleza maamuzi ya Baraza la Shura la kikundi.
Uongozi wa Hizbullah
Nasrallah alikua katibu mkuu wa Hezbollah mnamo Februari 16, 1992, kufuatia mauaji ya mtangulizi wake Abbas al-Musawi katika shambulio la anga la Israeli.
Chini ya uongozi wa Nasrallah, Hezbollah ilianzisha mfululizo wa operesheni za kimkakati dhidi ya Israel, na kufikia kilele chake kuondoka kwa majeshi ya Israel kutoka kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kukalia kwa miaka 22.
Mnamo 2004, alichukua jukumu muhimu katika mazungumzo ya kubadilishana wafungwa na Israeli, na kusababisha kuachiliwa kwa mamia ya wafungwa wa Lebanon na Waarabu.
Jukumu lake katika kuhakikisha Israel inajiondoa kutoka kusini mwa Lebanon ndani ya nchi ilimpatia jina la "kiongozi wa upinzani," hasa baada ya makabiliano ya baadaye ya Hezbollah na Israel wakati wa Vita vya Lebanon mwaka 2006.
Hotuba kali na kujitolea kwake kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Israel, hasa katika kuwatetea Wapalestina, kuliimarisha zaidi umaarufu wake katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Umaarufu wake unashuka kutokana na msimamo wake wa kuisaidia serikali ya Syria
Hata hivyo, umaarufu wa Nasrallah ulipungua kutokana na uungaji mkono wa Hezbollah kwa utawala wa Syria dhidi ya vikosi vya upinzani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Syria, vilivyoanza mwaka 2011.
Ushawishi wake uliongezeka baada ya operesheni ya "Flood Al-Aqsa" iliyoanzishwa na makundi ya Palestina, ikiwa ni pamoja na Hamas na Islamic Jihad, dhidi ya makazi ya Israel karibu na Gaza mnamo Oktoba 7, 2023.
Mashambulizi ya Israel Gaza, ambayo sasa yanakaribia kuadhimisha mwaka wake wa kwanza, yamesababisha zaidi ya Wapalestina 137,000 kuuawa na kujeruhiwa.
Nasrallah alitangaza kufunguliwa mashambulio ya kusini mwa Lebanon kuunga mkono muqawama wa Palestina," na kuapa katika hotuba kadhaa kwamba juhudi hizo zitaendelea kutumika hadi vita huko Gaza vitakapomalizika.