Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amekutana na kiongozi wa utawala mpya wa Syria, Ahmad al Sharaa.
Mkutano wa Jumapili katika mji mkuu wa Syria, Damascus, unakuja wiki mbili baada ya Bashar al Assad, kiongozi wa Syria kwa karibu miaka 25, kupinduliwa katika operesheni ya radi na vikosi vya upinzani.
Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Nuh Yilmaz na Kaimu Msimamizi Mkuu wa Uturuki katika Ubalozi wa Damascus, Burhan Koroglu, pia walikuwa kwenye mkutano huo.
Esaad Hassan Shaibani, ambaye aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa serikali ya mpito ya Syria, pia alikutana na ujumbe wa Uturuki.
Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani kwa ajili ya Mashariki ya Kati pia alisafiri kwenda Damascus siku ya Ijumaa, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje. Alikutana na maafisa kutoka Hayat Tahrir al Sham (HTS) kujadili hitaji la mchakato wa kisiasa "jumuishi".
Mkutano huo unakuwa wa kwanza kati ya maafisa wa Marekani na HTS siku chache baada ya Assad kukimbilia Urusi baada ya makundi yanayopinga utawala kuchukua udhibiti wa Damascus Desemba 8, na kumaliza utawala wa Chama cha Baath, uliokuwa madarakani tangu 1963.