Zaidi ya Wasyria 25,000 huko Uturuki wamerejea nyumbani Syria tangu Bashar al Assad kupinduliwa na makundi yanayopinga utawala, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema.
"Idadi ya watu waliorejea Syria katika siku 15 zilizopita imepita 25,000," Ali Yerlikaya aliambia shirika rasmi la habari la Anadolu.
Uturuki ni nyumbani kwa karibu wakimbizi milioni nne waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2011 nchini Syria.
Ankara inawasiliana kwa karibu na utawala mpya wa Syria na sasa inaangazia kurejea kwa hiari kwa wakimbizi wa Syria kwani mabadiliko ya madaraka huko Damascus yatawaruhusu wengi wao kurejea nyumbani.
Yerlikaya alisema ofisi ya uhamiaji itaanzishwa katika ubalozi na ubalozi mdogo wa Uturuki Damascus na Aleppo ili kumbukumbu za Wasyria waliorejea zihifadhiwe.
Uturuki ilifungua tena ubalozi wake mjini Damascus, karibu wiki moja baada ya Assad kupinduliwa na makundi yanayopinga utawala, na miaka 12 baada ya kituo hicho cha kidiplomasia kufungwa mapema katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Yerlikaya alisema mtu mmoja kutoka kwa kila familia atapewa haki ya kuingia na kutoka mara tatu kuanzia Januari 1 hadi Julai 2025 chini ya kanuni zitakazotungwa kutokana na maagizo ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Wasyria wanaorejea nchini mwao wataweza kuchukua mali zao na magari pamoja nao, aliongeza.