Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imethibitisha kifo cha kiongozi wa kikundi cha kigaidi cha Fetullah (FETO), Fetullah Gulen, katika hospitali nchini Marekani.
“Kiongozi wa FETO, ambaye aliwapumbaza watu wengi na kusuka mipango dhidi ya uhuru wa taifa la Uturuki, akisababisha matatizo kwa nchi yetu na jeshu letu, amekufa,” ilisema taarifa ya wizara hiyo siku ya Jumatatu.
“Japo amekufa, mtu huyu atakumbukwa kwa kushindwa kuona mateso ya watu wetu, na hili ni fundisho kwa wale wengine wenye nia ya kusaliti yao,” taarifa hiyo ilisisitiza.
Gulen, mwenye umri wa miaka 83, amekuwa akiishi kwenye jimbo la Pennsylvania nchini Marekani, kabla ya kufariki dunia katika hospitali ya Mtakatifu Luka nchini humo. Kwa muda mrefu, viongozi wa Uturuki wametaka arudishwe nchini ili ahukumiwe, bila mafanikio yoyote.
FETO na Fethullah Gulen aliyekuwa akiishi nchini Marekani, walisuka mipango ya mapinduzi ya Julai 15, 2016 nchini Uturuki ambapo watu 252 waliuwawa na wengine 2,734 kujeruhiwa. Ankara pia imeituhumu FETO kwa kuhusika na kampeni za kuipundua serikali kupitia taasisi mbalimbali za Uturuki, hususani mahakama, jeshi la ulinzi na jeshi la polisi.
“"Wale wenye mawazo ya kusaliti nchi yao wachukue mfano wa hili tukio na wajisalimishe wenyewe, kwenye taasisi za haki za Uturuki mapema iwezekanavyo,” ilisema wizara ya ulinzi kupitia taarifa yake.
Ankara ilitumia nafasi hiyo kuwakumbuka wale waliouwawa na magaidi, hususani wale wale waliouwawa Julai 15 (2016).
Wizara hiyo iliapa kwamba mapambano ya Uturuki dhidi ya makundi ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na FETO, yataendelea kwa dhamira na azimio "hadi mizizi yao itakapotokomezwa."