Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameipongeza serikali ya Iraq kwa jitihada zake za kupambana na kikundi cha kigaidi cha PKK, kinacholenga kutekeleza mashambulizi ya mpakani nchini Uturuki kutoka maficho yake kaskazini mwa Iraq.
Erdogan alioneshwa kuridhishwa na "hatua chanya," ikiwemo ya kukitangaza kikundi hicho kama shirika haramu, wakati akiwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani jijini Istanbul siku ya Ijumaa.
Viongozi hao walijadiliana uhusiano wa nchi mbili, na mambo mengine ya kikanda na ya ulimwenguni, kulingana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Erdogan alisisitiza kuwa kikundi hicho cha kigaidi kinahatarisha usalama wa Uturuki na Iraq, akiweka bayana kuwa, kukabiliana na ugaidi kutaimarisha amani na usalama katika nchi hizo mbili.
Aliongeza kuwa kuendeleza uhusiano na kutathmini fursa za ushirikiano, hasa Mradi wa Maendeleo ya Barabara, utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi zote mbili, ambazo zina uhusiano wa kina wa kihistoria na kiutamaduni
Rais wa Uturuki pia alishutumu kuongezeka kwa uvamizi wa Israeli katika eneo hilo, akisema kuwa na kutaja kuwa ni tishio kwa amani ya kikanda na kimataifa, na kusisitiza haja ya mshikamano, hasa kati ya nchi za kikanda, ili kukabiliana na tishio hilo.
Uratibu wa pamoja wa kiulinzi
Mwezi huu wa Agosti, nchi hizo mbili zilitia saini kile Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alichokiita makubaliano ya "kihistoria" kuhusu usalama, ushirikiano wa kijeshi na kukabiliana na ugaidi.
Mkataba huo, wa kwanza wa aina yake katika historia ya Uturuki na Iraq, uliashiria hatua muhimu katika uhusiano wa nchi mbili.
Nchi hizo mbili zinafanya kazi ya kuanzisha kituo cha pamoja cha kuratibu usalama mjini Baghdad na kituo cha pamoja cha mafunzo na ushirikiano katika eneo la Bashika, ambacho kitarahisisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi - hasa PKK.
Kundi hilo lina makao yake makuu kaskazini mwa Iraq, karibu na mpaka wa Uturuki, katika maeneo yaliyo chini ya Serikali ya kanda ya Wakurdi.
Katika kampeni yake ya zaidi ya miaka 40 ya ugaidi dhidi ya Uturuki, PKK - iliyoorodheshwa kama shirika la kigaidi na Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya- imehusika na vifo vya zaidi ya watu 40,000, ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto na wachanga.