Uturuki imetangaza siku moja ya maombolezo kitaifa itakayofanyika siku ya Jumatano kufuatia mkasa wa moto katika jiji la Bolu na kuua takribani watu 66, kulingana na Rais Recep Tayyip Erdogan.
Rais Erdogan pia alituma salamu zake za rambirambi kwa familia za waathirika wa tukio hilo, akiwaombea nafuu ya haraka wale waliojeruhiwa. Pia, ameuhakikishia umma kuwa wale waliohusika na janga hilo, hususani kwa uzembe watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Huu ni wakati wa kuonesha mshikamano, umoja na huruma na si wakati wa mijadala ya kisiasa,” alisisitiza Erdogan husu akitoa rai kwa sekta zote wakiwemo wanasiasa, vyombo vya habari na serikali za mitaa kuheshimu kipindi hicho cha maombolezo.
Rais alihitimisha kwa kuwaombea ustahimilivu na subiri familia zilizopoteza wapendwa wao akionesha tumaini kuwa Uturuki itakuwa salama dhidi ya majanga kama hayo siku za usoni.
Maafisa wanasema kuwa moto huo ulizuka kwenye ghorofa ya 12 katika hoteli maarufu kaskazinimagharibi mwa Uturuki mapema Jumanne na kuua watu 66.
Watu wapatao 51 walijeruhiwa katika tukio la moto lililotokea katika hoteli ya Grand Kartal katika eneo la Kartalkaya, jimboni Bolu, takribani kilomita 300 kutoka Mashariki mwa jiji la Istanbul.
Usitishwaji wa vita vya Gaza, Syria
Kuhusu suala la Syria, Erdogan amezitaka jumuiya za Kiarabu na Kiislamu kusaidia ujenzi wa Syria kabla ya mataifa ya Magharibi kuanza kuondoa vikwazo kwa nchi hiyo.
Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Jumanne.
Kuhusu usitishwaji wa vita vya Gaza, Erdogan alisema kuwa taswira za ubadilishanaji wafungwa zinaonesha yule anathamini tunu za utu na mwenye kudharau tunu hizo, alisema Erdogan akiikosoa Israeli.
“Ndugu zetu wa Gaza wamelipa gharama kubwa, lakini hawatojisalimisha kwa kwa wahuni na sera za mauaji,” aliongeza.
Uturuki itaongeza kasi ya jitihada za upatikanaji amani ndani ya kanda, “usitishwaji wa vita ukiwa kama fursa”, aliongeza.