Ankara imeweka msisitizo juu ya umuhimu wa UNIFIL katika kuimarisha amani ya kikanda baada ya shambulizi baya la Israeli huko Lebanon./ Picha: AA  

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imelaani shambulizi la Israeli dhidi ya kambi ya mpito ya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) na kuionya Israeli iache mpango wake wa kuendelea kuikalia kimabavu Lebanon.

Katika taarifa yake, Wizara hiyo imeweka msisitizo juu ya umuhimu wa UNIFIL katika kuimarisha amani ya kikanda baada ya shambulizi baya la Israeli huko Lebanon.

"UNIFIL ilitumwa hapo kuimarisha usalama wa kikanda. UNIFIL ina umuhimu mkubwa sana hasa katika kipindi ambacho Israeli imenuwia kusambaza vita zaidi katika kanda hiyo."

Wizara hiyo, pia imetabanaisha kuwa , "mashambulizi ya mara kwa mara ya Israeli, ni ushahidi wa sera ya serikali ya Netanyahu ya kuikalia Lebanon na kutumia silaha katika mazingira yoyote yale."

Ankara pia imetoa wito kwa nchi zote kuungana na kutoa msimamo wa pamoja dhidi ya Israeli na nchi zinazoipa silaha.

"Kila mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ana wajibu wa kuzuia mashambulizi ya Israeli dhidi ya majeshi ya Umoja wa Mataifa."

Shambulio la Israeli dhidi ya UNIFIL

Siku ya Jumapili, walinda usalama wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon walisema kuwa vifaru vya Israeli vilivunja geti katika upande wa mpaka wa Lebanon, baada ya kuzuia njia yake siku iliyotangulia.

Tukio hilo linakuja baada ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kumtaka mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwahamisha wanajeshi wa kulinda amani waliotumwa kusini mwa Lebanon akidai kuwa Hezbollah inawatumia kama "ngao za binadamu".

UNIFIL imekataa kuondoka kusini mwa Lebanon.

TRT Afrika