Uturuki imeazimia kulinda "makundi yote yaliyoathirika" nchini Syria, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo amesema.
"Iwe ni wengi au wachache nchini Syria, yeyote yule - Nusayris, Alevis, Yazidis, Wakristo, mtu yeyote - Uturuki ndiye mlinzi na msimamizi wao kama ilivyo kwa wengine wote katika kipindi hiki kipya," Hakan Fidan alisema hayo kwenye mkutano wa pamoja na mwenzake wa Ubelgiji Bernard Quintin jijini Ankara siku ya Alhamisi.
Alisema wakati wa ukandamizaji wa utawala wa Assad, mamilioni ya Waarabu wa Kisunni walifukuzwa, pamoja na makabila ya Waturuki , na ilibidi kutafuta hifadhi katika nchi nyingine.
Fidan alisisitiza kuwa Uturuki haikusita kuwakubali wale wanaotafuta hifadhi kukimbia ukandamizaji.
Tangu 2011, nchi hiyo imetoa hifadhi kwa zaidi ya Wasyria milioni 3. Fidan alisema Ankara haijawahi kusita kushiriki mzigo wa wale wanaotafuta hifadhi na kuchukua hatua za kuhakikisha wanaishi kwa amani katika siku zijazo za Syria.
"Tunafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba hawakabiliwi na madhara nchini Syria. Uongozi mpya wa Syria pia unajali sana suala hili," aliongeza waziri huyo.
Mustakabali wa Syria
"Tunatumai na tunatamani kwamba watu wa Syria watajenga mustakabali wao haraka," Fidan alisisitiza.
Alisisitiza kuwa ujenzi mpya wa Syria unahitaji msaada wa kimataifa, na Ankara imejitolea kusaidia usalama wa nchi, uhifadhi wa mamlaka yake ya ardhi, na juhudi za kujenga upya.
Fidan pia alizungumzia mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza, akisisitiza kwamba yanatishia sio tu Wapalestina bali pia mfumo wa kimataifa, akitaka kukomeshwa mara moja kwa uhalifu huo.
Kuhusu wafungwa wa Daesh nchini Syria, Fidan alisisitiza tena msimamo wa Uturuki kwamba wanamgambo wa kigeni wanapaswa kurejeshwa katika nchi zao, na kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kutatua suala la kuwekwa kizuizini kwa njia ambayo itazuia migogoro zaidi.
Alisisitiza utayar wa Uturuki kuunga mkono Syria katika kulinda kambi na magereza na kuhakikisha uhifadhi wa mamlaka ya mipaka ya nchi hiyo.
Mahusiano ya Uturuki na Ubelgiji
Akizungumzia uhusiano na nchi ya Ubelgiji, Fidan amesisitiza ya kwamba nchi hizo ni washirika wa NATO, zina urafiki wa muda mrefu, na uhusiano unaokua wa kibiashara na uwekezaji.
Amesema nchi zote mbili zinalenga kuendeleza ushirikiano wa sekta ya ulinzi na kuimarisha zaidi uhusiano kati ya makampuni ya Uturuki na Ubelgiji.
Alisema walijadili mada kama vile uungaji mkono wa Ubelgiji kwa uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya, umoja wa forodha, urahisishaji wa visa, na masuala mengine.
Fidan pia alielezea wasiwasi wake juu ya kuwepo kwa PKK, FETO na makundi mengine ya kigaidi nchini Ubelgiji, akihimiza jitihada za kuzuia matumizi mabaya ya sheria za ndani.