Uturuki itaendelea kushirikiana na Misri kutoa misaada ya kibinadamu na chakula kwa Gaza ya Palestina, balozi wa Uturuki mjini Cairo amesema.
Hakuna njia mbadala ya Misri katika kupeleka misaada ya kibinadamu kwa Gaza iliyozingirwa, ambayo nchi hiyo inapakana, Salih Mutlu Sen alisema katika hafla ya kifungua kinywa katika Ubalozi wa Uturuki Jumanne.
Akinukuu taarifa za maafisa wa Umoja wa Mataifa, Sen alibainisha kuwa asilimia 95 ya misaada iliyotumwa Gaza, hasa ya chakula, ilitolewa kupitia Misri kupitia Kivuko cha Mpakani cha Rafah - sehemu pekee ya kuingia au kutoka Gaza ambayo Israel haidhibiti.
Akielezea matumaini yake kuwa hali ya usalama katika mpaka itaimarika haraka iwezekanavyo ili kurahisisha misaada zaidi kwa Gaza, alisema Israel, ambayo ilianzisha mashambulizi ya ardhini dhidi ya Rafah licha ya onyo la kimataifa, ndiyo iliyosababisha kuzorota kwa sasa.
Jeshi la Israel linapaswa kuondoka kutoka upande wa Palestina wa Kivuko cha Mpakani cha Rafah, ambacho kiliukalia kinyume cha sheria mapema mwezi huu, alisema Sen, akisisitiza kuwa Uturuki na Misri zilidai hivyo.
Amesisitiza kuwa, ziara za ngazi ya juu kati ya Uturuki na Misri zitaendelea kuongezeka katika kipindi kijacho na kuongeza kuwa njia za ushirikiano na mshikamano hasa Palestina ndizo zitakazoongoza ajenda.
Zaidi ya Wapalestina 35,600 waliuawa
Israel imeendeleza mashambulizi yake ya kikatili huko Gaza licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika eneo hilo.
Zaidi ya Wapalestina 35,600 wameuawa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na karibu wengine 79,900 kujeruhiwa tangu Oktoba mwaka jana kufuatia shambulio la kundi la muqawama la Palestina Hamas.
Zaidi ya miezi saba ya vita vya Israel, maeneo makubwa ya Gaza yalikuwa magofu huku kukiwa na kizuizi cha chakula, maji safi na dawa.
Israel inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo imeiamuru kuhakikisha kuwa vikosi vyake havifanyi mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia huko Gaza.