Waziri wa Ulinzi wa Uturuki alionesha masikitiko yake kwa Iraq kushindwa kutambua marufuku dhidi ya kikundi cha kigaidi cha PKK./Picha:AA

Uturuki imeazimia kushirikiana na Iraq, ikiwemo kuanzisha operesheni ya pamoja, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Yasar Guler, amesema.

Kufuatia ziara yake kwenye mji mkuu wa Iraq wa Baghdad, serikali ya Iraq ilichukua maamuzi ya kukipiga marufuku kikundi cha PKK na kwa mara ya kwanza kukiita kama kikundi cha kigaidi.

“Tutafanya kazi pamoja baada ya hatua hii. Tutaanzisha kituo cha operesheni za pamoja,” alisema Guler siku ya Jumatano wakati alipotembelea jimbo la Kahramanmaras lililoko kusini mwa Uturuki, ambapo pia alimtembelea gavana wa eneo hilo Mukerrem Unluer.

Guler alisema ugaidi ni janga la Uturuki, akionesha kuwa ni changamoto kubwa kwa nchi, na kusisitiza ustahimilivu wa taifa hilo.

“Tunaishi katika eneo ghali zaidi duniani. Kutakuwa na gharama za kulipa. ... Tuna kila aina ya madini. Tuna rasilimali watu. Bila shaka, hii inasumbua kila mtu. Zaidi ya hayo, maendeleo na ukuaji wa kasi wa nchi yetu katika miaka ya hivi karibuni, hasa katika miaka 20 iliyopita, unasumbua kila mtu anayetuzunguka,” alisema.

Pia alisisitiza kuwa baadhi ya makundi yanayotatizwa na ukuaji wa kasi wa Uturuki yanatumia vikundi vya kigaidi kuzorotesha hali hii na kwamba ni lazima nchi iwe na nguvu kila wakati.

Msimamo chanya wa utawala wa Erbil

Kuhusu mgogoro wa miongo minne wa kikundi cha PKK, Guler alionesha masikitiko yake kwa Iraq kushindwa kutambua marufuku dhidi ya kikundi cha kigaidi cha PKK.

“Tumekuwa tukipambana na kikundi cha kigaidi cha PKK kwa miaka 40. Lakini kwa bahati mbaya, kwa miaka 40, serikali ya Iraq imeshindwa kuwaita wao magaidi au kukipiga marufuku. Kikundi hicho kiko kwenye nchi yao na hawaoneshi kubugudhiwa nacho,” alisema.

“Tulikuwa na kikao mjini Ankara Disemba. Suala hilo lilitiliwa mkazo sana kwenye mkutano huo na tulivyoenda Iraq na katika ziara yetu ya mwisho nchini Iraq, serikali ya Iraq ilikubali na kwa mara ya kwanza walikiita kikundi cha PKK kuwa cha kigaidi," alisema.

Akigusia msimamo chanya wa utawala wa Erbil, Guler pia alisisitiza kuwa juhudi zilizoko ziwe zaidi ya kupambana na ugaidi.

“Kutakuwa na tume mpya kuhusu nishati, kilimo, ufugaji, maji na mambo mtambuka, na tutaendelea jitihada zetu za kufikia maendeleo katika nyanja zote za ushirikiano wetu,” alisema.

Pia aligusia umuhimu wa maendeleo ya mradi wa barabara unaounganisha eneo la ghuba hadi Ulaya, kupitia Uturuki.

“Hili ni jukumu muhimu sana kwa mustakabali wa Uturuki. Kupitia mradi huu, makampuni yote ya Uturuki yatachagua kufanya biashara pale. Pamoja na barabara ya njia nne, reli nne, bidhaa zote kutoka China zitakuwa zikisafirishwa Ulaya kupitia Barabara hiyo ya Maendeleo,” alisisitiza Guler.

TRT Afrika