Uturuki iko tayari kutoa msaada wa aina yoyote kumaliza uhasama kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, iwapo pande hizo zitahitaji msaada huo, Rais Recep Tayyip Erdogan amesema
“Sisi, kama Uturuki tuko tayari kusaidia kwa njia yoyote ile kumaliza mgogoro kati ya Rwanda na DRC, hatua ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa amani na utulivu katika kanda ya Maziwa Makuu, iwapo tu nchi hizo zitaridhia,” alisema Erdogan siku ya Alhamisi, katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na mgeni wake Rais Paul Kagame jijini Ankara.
Tangu mwaka 2022, kikundi cha waasi cha M23 kimeendeleza machafuko katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Kinshasa na nchi zingine zimeishutumu Rwanda kwa kukisaidia kikundi hicho, tuhuma ambazo zimepingwa na Kigali.
Erdogan pia alipongeza jitihada za Rwanda za kukabiliana na shirika la kigaidi la FETO.
FETO iliongoza mapinduzi yaliyoshindwa ya Julai 15, 2016 ambayo yalisababisha vifo vya watu 252 na majeruhi 2,734 nchini Uturuki.
Uturuki inaituhumu FETO kwa kushiriki katika kampeni ya kuipindua serikali kupitia kujipenyeza ndani ya taasisi za Uturuki, hususani jeshi, polisi na mahakama.