Maonesho yasiyo ya kimadili siku ya ufunguzi wa michuano ya Olimpiki ya Paris yamesababisha hasira na kuibua majibu, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemwambia Kiongozi wa Vatican, Papa Francis kwa njia ya simu.
"Rais Erdogan alisema kuwa chini ya mwamvuli wa uhuru wa kujieleza na kuvumiliana, utu wa binadamu ulikanyagwa na maadili ya kidini na kimaadili yalidhihakiwa, jambo ambalo liliwaudhi Waislamu kama ilivyoudhi ulimwengu wa Kikristo," ilisema Kurugenzi ya Mawasiliano ya Jamhuri ya Uturuki kwenye ukurasa wake wa X siku ya Alhamisi.
Rais wa Uturuki alisisitiza haja ya kupaza sauti ya umoja na kuchukua msimamo mmoja dhidi ya vitendo hivi, ilisema taarifa hiyo.
"Rais Erdogan aligusia kuwa changamoto kwenye tunu za dini na uenezwaji wa taarifa potofu wakati wa michezo ya Olimpiki, ambayo inalenga kuwaunganisha watu, ni za kushtua na inaonesha upotevu wa maadili," iliongeza tarifa hiyo.
'Israeli ni tishio kwa kanda nzima'
Katika mazungumzo ya simu, Rais Erdogan pia alibainisha kwamba "mashambulizi ya Israeli dhidi ya Gaza yamegeuka kuwa mauaji ya kimbari," yakisababisha mgogoro, matatizo na maafa makubwa ya kibinadamu, na kwamba "Israeli ilitekeleza mauaji haya chini ya mwamvuli wa kidiplomasia, kiuchumi, na kijeshi uliotolewa na baadhi ya mataifa."
"Rais Erdogan alisema kuwa mauaji ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh na shambulio la Lebanon yanaonyesha tena kwamba Israeli ni tishio kwa kanda nzima, dunia, na ubinadamu," ilisema taarifa hiyo.
Erdogan pia alisisitiza umuhimu wa muungano wa kibinadamu kuchukua hatua bila kuchelewa ili kuhakikisha amani kwa Waislamu na Wakristo wanaoishi Palestina.
"Rais Erdogan alieleza imani yake kwamba mazungumzo ya Papa Francis na nchi zinazounga mkono Israeli, ili kusitisha mashambulizi na kufanikisha amani ya kudumu, yatakuwa na manufaa kabla ya madhara ya kudumu kufanywa kwenye usalama wa kisiasa, na muundo wa kijamii wa kanda na dunia," ilisema taarifa hiyo.
Wakati wa mazungumzo hayo, Papa Francis alimshukuru Rais Erdogan kwa juhudi zake za kutafuta amani.