Uturuki na Misri zina msimamo mmoja kuhusu suala la Palestina, na pande zote mbili zinataka kuona usitishaji wa vita vya Israeli dhidi ya Gaza mara moja na wa kudumu, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema.
"Michango ya Uturuki na Misri kwa amani na utulivu wa kikanda ni muhimu sana," Erdogan alisema Jumatano, akihutubia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Misri Abdel Fattah el Sisi, ambaye yuko ziarani Uturuki.
Hii ni mara ya kwanza kwa Sisi kuzuru Uturuki tangu aingie madarakani mwaka wa 2014. Ziara hiyo inakuja baada ya kupata mwaliko wa Erdogan.
Kama sehemu ya ziara ya Sisi, viongozi hao waliongoza kikao cha kwanza cha Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati wa Ngazi ya Juu kati ya nchi hizo mbili na kusaini mikataba 18 katika nyanja mbalimbali.
"Tumethibitisha tena nia yetu ya kuendeleza ushirikiano wetu katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na viwanda, biashara, ulinzi, huduma za afya, mazingira na nishati," Erdogan alisema, akiongeza kuwa nchi hizo mbili zitaendeleza uhusiano wao wa nyanja nyingi kwa njia kunufaishana."
Historia ya pamoja, uhusiano wa karibu
Uturuki na Misri, nchi mbili zenye nguvu za Mashariki ya Kati, zimekuwa zikisonga mbele kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha uhusiano ulioanzishswa miaka mitatu iliyopita.
Mwezi Februari, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitembelea Misri, ambako alikutana na Sisi na kutia saini mikataba kadhaa kuhusu utalii, utamaduni na elimu.
Uhusiano wa kibiashara kwa muda mrefu umekuwa msingi wa ushirikiano kati ya Uturuki na Misri.
Nchi hizo mbili sasa zinatumai kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kwa angalau asilimia 50, kutoka dola bilioni 10 hadi dola bilioni 15.
Uturuki imekuwa miongoni mwa washirika wakuu watano wa biashara wa Misri kwa miaka 10 iliyopita.
Nchi hizo mbili zinajivunia karne nyingi za historia ya pamoja na uhusiano wa karibu wa urafiki.
Mwaka ujao ni miaka 100 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati yao.