Shirika la ndege la Uturuki, Turkish Airlines (THY) limetangaza kusitisha huduma za ndege kwenda Israel kutokana na matukio ya hivi majuzi katika eneo hilo. / Picha: AA

Shirika la ndege la Ututurki - Turkish Airlines (THY) limetangaza kusitisha huduma za ndege kwenda Israel kutokana na matukio ya hivi majuzi katika eneo hilo.

"Kwa sababu ya hali ya sasa nchini Israeli, safari zetu za ndege zimesitishwa hadi ilani nyingine," Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Mahusiano ya Vyombo vya Habari Yahya Ustun alisema Jumanne katika mtandao wa -X.

Mashirika mengine mengi ya ndege pia yamesitisha au kupunguza sana huduma kwa Israel.

Israel iliendelea na mashambulizi yake ya anga kwenye Ukanda wa Gaza kwa siku ya tatu Jumanne, kufuatia mashambulizi ya makundi mbalimbali ya Hamas kwenye miji ya Israel karibu na eneo la bahari.

Hamas ilisema shambulio hilo lilitokana na ukiukaji wa sheria za Israel katika eneo la Msikiti wa Al Aqsa katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Jerusalem Mashariki na kuongezeka kwa ghasia za walowezi.

Israel ililipiza kisasi kwa mfululizo wa mashambulizi ya anga kwenye Gaza na kuweka vizuizi kamili katika eneo hilo, ambalo ni makazi ya karibu watu milioni 2.3.

Israel yazidisha mashambulizi yake Gaza

Jeshi la Israel lilisema Jumanne lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga yaliyolenga zaidi ya shabaha 100 huko Gaza. Jeshi lilisema kuwa vikosi vyake viliwaua wapiganaji wanne wa Kipalestina waliokuwa wamejaribu kujipenyeza Israel karibu na Zikim karibu na Gaza.

Wanajeshi wa Israel walishambulia boti za wavuvi za Wapalestina katika Bandari ya Gaza, na kuacha idadi ya boti zikiwaka moto.

Jeshi pia lilisema Juad Abu Smallah, waziri wa uchumi wa Hamas huko Gaza, aliuawa katika shambulio la anga katika mji wa Khan Younis.

Hamas, kwa upande wake, ilithibitisha Jumanne kwamba maafisa wake wawili waliuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza. Kundi hilo lililipiza kisasi kwa kurusha roketi katika miji ya kati ya Israeli, ikiwa ni pamoja na Ashkelon, Tel Aviv, Beersheba na Rishon LeZion.

Hamas ilisema kuwa imeshambulia Ashkelon kwa mamia ya maroketi kujibu kuhama kwa raia huko Gaza. Harakati ya Wapalestina pia ilisema ilirusha makombora yaliyolenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion.

Zaidi ya watu 1,800 wameuawa katika ongezeko hilo tangu Jumamosi, wakiwemo zaidi ya Waisraeli 1,000.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kutumia nguvu zote za Israel kuharibu uwezo wa Hamas na "kulipiza kisasi kwa siku hii nyeusi."

TRT Afrika