Kumetokea shambulio la kigaidi katika makao makuu ya kiwanda cha Turkish Aerospace (TAI) kilichopo kwenye mji mkuu wa Ankara, Taarifa zinasema kulisikika mlipuko mkubwa huku picha mjongeo zikionesha majibizano ya risasi.
"Kwa bahati mbaya, idadi ya mashahidi imefikia watano huku waliojeruhiwa wakiwa ni 22," Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya aliwaambia wanahabari siku ya Jumatano.
Huduma za dharura za uokoaji zilielekezwa eneo la tukio, huku picha mjongeo zikionesha geti lililoharibiwa na majibizano ya silaha yakiendelea karibu na eneo la kuegeshea magari.
Yerlikaya hakutaja jina la shirika lililohusika na shambulio hilo, huku mchakato wa kuwatafuta waliotekeleza tukio hilo ukiendelea. Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi Yasar Guler ameelekezea kidole cha lawama kikundi cha kigaidi cha PKK.
“Kila wakati, tunawapa wahuni wa PKK adhabu wanazostahili. Lakini ni kama hawaelewi,” alisema Guler.
“Tutaendelea kuwasaka mpaka gaidi wa mwisho anaangamizwa.”
Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Umma ya jijini Ankara imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.
TAI ni mojawapo ya makampuni muhimu ya ulinzi na usafiri wa anga ya Uturuki. Inazalisha KAAN, ndege ya kwanza ya kitaifa ya kivita nchini humo, miongoni mwa bidhaa nyingine.
Hukumu kutoka ulimwengu mzima
Tukio hilo limepokelewa na lawama kutoka pande mbali mbali za dunia.
Rais wa Urusi alikuwa kiongozi wa kwanza kulaani shambulizi hilo na alitoa salamu za rambirambi kwa Rais wake wa Uturuki Erdogan ambaye yuko Kazan kuhudhuria Mkutano wa BRICS.
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia wamelaani shambulio hilo.
"Tunalaani vikali ugaidi wa aina zote na tunafuatilia kwa karibu maendeleo," Rutte alisema kwenye ukurasa wake wa X.
Guterres pia alituma salamu zake za rambirambi kwa Uturuki.
"Tunasubiri taarifa lakini tunalaani shambulizi hili dhidi ya raia. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia za wahasiriwa na tunatumai kupona kamili kwa waliojeruhiwa," naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq alisema kwa niaba ya Guterres.
Nchi ya Pakistan ililaani vikali shambulio hilo la kigaidi.
Akitoa salamu zake za rambirambi kwa waliopoteza maisha, Rais Asif Zardari alionyesha mshikamano wake na serikali na watu wa Uturuki.
"Pakistani ilisimama kwa mshikamano kamili kwa ndugu zetu wa Uturuki katika kipindi hicho kigumu. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia za wale waliopoteza maisha katika shambulio hili huku tukiwaombea nafuu ya haraka majeruhi wote," alisema Zardari.
Algeria na Jordan pia ni miongoni mwa nchi zilizolaani shambulio hilo.
'Marekani yalaani vikali tukio hilo la kigaidi'
Utawala wa Biden umelaani vikali shambulio baya la kigaidi kwenye makao makuu ya kiwanda cha anga cha Uturuki (TAI) kilichopo jijini Ankara.
Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House John Kirby alisema kuwa mawazo ya Washington yapo kwa "waathirika wa shambulio baya la kigaidi huko Ankara, Uturuki."
"Asubuhi ya leo, sala zetu ziko pamoja na wale wote walioathiriwa na familia zao, na bila shaka, pia watu wa Uturuki katika kipindi hichi kigumu," aliwaambia waandishi wa habari.
"Mamlaka ya Uturuki, kama walivyosema, wanachunguza hili kama shambulio la kigaidi linalowezekana, na wakati hatujui nia gani au ni nani haswa anayehusika, tunalaani vikali kitendo hiki cha vurugu," aliongeza.