Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesisitiza kuwa mapigano mapya huko Aleppo nchini Syria ni matokeo ya masuala ambayo hayajatatuliwa kwa muda mrefu, na sio uingiliaji kati wa nje.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi jijini Ankara, Fidan alihusisha kuzuka upya kwa ghasia na kukataa kwa utawala wa Syria kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa.
Amesisitiza kuwa, matukio ya hivi karibuni ni ushahidi kwamba utawala wa Syria lazima upatane na watu wake na upinzani.
Fidan alisisitiza msimamo wa Ankara wa kuzuia kuongezeka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, ambavyo vimeanza tangu 2011.
Mapigano kati ya vikosi vya utawala wa Assad na makundi ya upinzani yenye silaha yanaashiria kuongezeka tena kwa mzozo baada ya muda wa utulivu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ambaye yuko katika ziara rasmi nchini Uturuki, alieleza kuungana na Ankara katika masuala muhimu ya kikanda na changamoto zilizopo.
Akiangazia majadiliano juu ya kuunga mkono usitishaji vita wa Ghaza, kushughulikia utoaji wa misaada ya kibinadamu, na kukabiliana na "hujuma zinazofanywa na utawala wa Kizayuni," Araghchi pia alisisitiza kwamba matatizo mengi ya eneo hilo yanatokana na uingiliaji kati wa kigeni.
Mawaziri wote wawili walisisitiza kujitolea kwao kwa mazungumzo na ushirikiano ili kushughulikia masuala ya kibinadamu nchini Syria na eneo zima.