Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amejadili uhusiano wa nchi mbili, migogoro ya kikanda na maendeleo ulimwenguni katika mazungumzo yake ya simu na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud.
Wakati wa mazungumzo hayo siku ya Jumapili, Rais Erdogan alisisitizia umuhimu wa ushirikiano kati ya Uturuki na Somalia, akiangazia ushrikiano wa nchi hizo mbili, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki imesema katika ukurasa wake wa X.
Rais huyo wa Uturuki amehakikisha kuwa Uturuki itaendelea na jitihada zake za kusuluhisha mvutano kati ya Somalia na Ethiopia.
Uturuki mwenyeji wa mazungumzo
Duru ya awali ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Ethiopia na Somalia ilifanyika katika mji mkuu wa Uturuki Ankara mapema Julai. Kutokana na hali hiyo, vyama hivyo vilikubaliana kukutana tena kwa duru ya pili Septemba 2.
Akielezea matumaini kuhusu duru ya pili ya mazungumzo, Erdogan alimwambia mwenzake wa Somalia kwamba Uturuki inatarajia kuona matokeo chanya kutoka kwenye mazungumzo hayo.
Siku ya Jumamosi, Erdogan alikuwa na mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambapo aliangazia hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Ethiopia kuondoa hofu ya Somalia juu ya utawala wake.