Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Israeli inayoendelea kushambulia kwa mabomu Gaza na Lebanon ni "shirika la kigaidi la Kizayuni."
Erdogan aliuambia mkutano wa chama tawala cha Haki na Maendeleo (AK) Party mjini Ankara kwamba tangu mwaka jana, Israeli imekuwa ikitenda kama "shirika la kigaidi" badala ya taifa.
Alisema Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na "mtandao wake wa mauaji ni wa udanganyifu na wanaanza mwenendo hatari sana."
Rais wa Uturuki aliionya Israeli kwamba "udanganyifu wake wa ardhi ya ahadi" hatimaye utasababisha kuvunjika kwa moyo.
Aliapa Uturuki kamwe haitahatarisha usalama wake na kuruhusu matarajio ya upanuzi katika eneo hilo kutimia.
Erdogan pia alizikosoa nchi za Magharibi kwa kuendelea kutoa silaha kwa Israeli.
"Historia haitawasamehe kamwe wale wanaompongeza mkatili mkubwa aliyehusika na damu ya makumi ya maelfu ya watoto, wanawake na raia wa Palestina," alisema.
Pia alitoa wito wa kuongezeka kwa mazungumzo ya kikanda, akisema: "Kwa kuzingatia hali ilivyo katika eneo letu, tunaamini kwamba tunahitaji kuzungumza zaidi, tunahitaji maridhiano."
Erdogan amewapongeza Wapalestina kwa ustahmilivu wao akisema: "Tunajua vizuri sana kwamba watu wa Palestina pia wanatetea ubinadamu, kutetea heshima ya Waislamu."
Israeli inaendelea na mashambulizi yake ya angani na ardhini dhidi ya Lebanon huku pia ikifanya mashambulizi huko Gaza, ambapo imeua zaidi ya Wapalestina 41,000 tangu mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israeli tarehe 7 Oktoba 2023.