Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameitaka jumuiya ya kimataifa kuheshimu matakwa ya watu wa Gaza.
“Serikali ya Israeli isiruhusiwe kukiuka usitishwaji huu,” alisema Erdogan katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa Mongolia Ukhnaa Khurelsukh katika mji mkuu wa Ankara siku ya Alhamisi.
Ulimwengu ni lazima uwajibike katika suala la Palestina,” alisema Erdogan.
“Licha ya kupoteza zaidi ya mashahidi 50,000, wengi wakiwa ni watoto na wanawake, Gaza haikukata tamaa wala kusalimu amri kwa wadhalimu hao,” alisisitiza Erdogan.
“Kama ushirika wa kibinadamu, ni lazima tufanye bidii, hususani kuanzia hatua hii kuhakikisha kuwa tunatilia mkazo usitishwaji wa vita vya Gaza ili kutibu majeraha ya eneo hilo,” alibainisha.
“Uturuki inaamini katika mazungumzo ya amani kuelekea kuundwa kwa taifa la Kipalestina lenye mji mkuu wa Yerusalemu Mashariki, mapema iwezekanavyo,” aliongeza Erdogan.
Kwa upande wake, Khurelsukh aliishukuru Uturuki kwa jitihada zake za kuleta amani katika ngazi ya kanda na ulimwengu mzima.
Kufikia makubaliano ya kusitisha vita
Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Qatar na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alitangaza kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza, huku akisema huku utekelezwaji wa mpango huo unategemewa kuanza Jumapili hii.
Maafikiano hayo yanakuja siku 467 baada ya kampeni katili ya Israeli dhidi ya Gaza, ambayo iliua zaidi ya watu 46,700 wengi wakiwa ni wanawake na watoto.
Watu wapatao 1,200 waliuwawa katika uvamizi wa Oktoba 7, 2023 huku wengine 250 wakichukuliwa kama mateka katika eneo la Gaza.