Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa mara nyingine ametoa wito kwa dunia kuwa katika upande sahihi wa historia, huku mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza ya Palestina yakiendelea baada ya mwezi mmoja.
"Ulimwengu unabaki kimya. Marekani na Magharibi zote ziko kimya," Erdogan alisema, akihutubia Mkutano wa 16 wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi siku ya Alhamisi.
Alibainisha kuwa karibu watu 11,000 wameuawa huko Gaza katika mwezi uliopita, asilimia 73 wakiwa ni wanawake na watoto.
Akisisitiza kwamba serikali ya Benjamin Netanyahu ingali inaendelea na kampeni yake ya kijeshi, Erdogan aliongeza:
"Utawala wa Israel unaendelea kushambulia kwa mabomu shule, misikiti, makanisa, hospitali na vyuo vikuu, na kukiuka maadili yote ya ubinadamu."
"Sisi kama Waislamu kama hatutapaza sauti zetu leo, tutafanya lini?" aliuliza Rais wa Uturuki.
Uturuki imekuwa mhusika mkuu katika juhudi za misaada, na imewasilisha ndege 10 zilizobeba zaidi ya tani 230 za misaada ya kibinadamu kuelekea Gaza kwenye Uwanja wa Ndege wa El Arish kwa msaada wa Misri, alisema.
Tangu Oktoba 7, Israel imewaua zaidi ya Wapalestina 10,500 katika mashambulizi ya mara kwa mara huko Gaza - makazi ya milioni 2.3.
Takriban asilimia 40 ya waliouawa ni watoto, kulingana na maafisa.