Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Israel lazima iache mipango yake ya kujitanua na kukumbatia suluhu ya mataifa mawili.
Akizungumza katika Mkutano wa Viongozi wa Serikali za Dunia mjini Dubai siku ya Jumanne, Erdogan alisema: "Iwapo Israel inataka amani ya kudumu, ni lazima iache kutekeleza azma yake ya kujitanua na ikubali kuwepo kwa taifa huru la Palestina linalozingatia mipaka ya 1967."
"Israel, ambayo inajiona kuwa juu ya sheria za kimataifa, haijaacha sera zake za uvamizi, unyakuzi, uharibifu na mauaji kwa miongo kadhaa," rais wa Uturuki alisema.
Pia alizitaka nchi "zinazozingatia" kuunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina au UNRWA, akilipongeza kama "njia ya kuokoa wakimbizi milioni 6 nchini Jordan, Syria, Lebanon na Palestina."
"Hatutawaacha ndugu zetu Wapalestina wakiwa wametelekezwa, wanyonge, au peke yao," aliongeza.
Ziara ya siku mbili ya UAE
Erdogan aliwasili Umoja wa Falme za Kiarabu mapema Jumanne kama sehemu ya ziara ya siku mbili kuhudhuria mkutano huo.
Atahutubia mkutano huo wa siku tatu, wenye kauli mbiu ya mwaka huu “Kuunda Serikali za Baadaye,” unaowaleta pamoja viongozi wa serikali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, wasomi, asasi za kiraia, wabobezi, vyombo vya habari na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali.
Vita vya Israeli dhidi ya Gaza tangu uvamizi wa mpaka wa kundi la Hamas tarehe 7 Oktoba, na kuua takriban watu 1,200, hujuma ya Israel huko Gaza imeua zaidi ya watu 28,000 na kusababisha uharibifu mkubwa na uhaba wa mahitaji.
Vita vya Israel dhidi ya Gaza vimesababisha asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo kuwa wakimbizi wa ndani huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, huku asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo ikiharibiwa, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Israel inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo katika uamuzi wa muda wa mwezi Januari iliiamuru Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu inatolewa kwa raia huko Gaza.