Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisisitiza tena kwamba hakuna nguvu inayoweza kuwalazimisha watu wa Gaza kutoka katika nchi yao "ya milele", kwani Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Jerusalem Mashariki ni mali ya Wapalestina.
"Hakuna aliye na uwezo wa kuwaondoa watu wa Gaza kutoka katika ardhi yao ya milele, ambayo imekuwepo kwa maelfu ya miaka. Palestina, ikiwa ni pamoja na Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Jerusalem Mashariki, ni ya Wapalestina," Erdogan aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumapili huko Istanbul kabla ya kuruka kuelekea Malaysia.
Mapendekezo ya utawala wa Marekani kuhusu Gaza, yaliyotolewa kwa shinikizo kutoka kwa utawala wa Kizayuni, hayafai kujadiliwa, alisema Erdogan, akizungumzia pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuwahamisha Wapalestina.
Erdogan pia aliipongeza Hamas kwa kutimiza ahadi zake katika mabadilishano ya wafungwa yanayoendelea na Israel, licha ya majaribio ya Israel kuhujumu mchakato huo.
Kuhusiana na hali ya Syria, Erdogan alisema kwamba makaburi ya halaiki yanafukuliwa katika maeneo tofauti ya Syria, uso wa umwagaji damu wa utawala wa Assad unafichuliwa.
Rais wa Uturuki alielezea matumaini ya utulivu wa Syria chini ya uongozi wa Rais Ahmed Alsharaa, akipendekeza nchi hiyo itapata amani hivi karibuni.
Hakuna nafasi kwa makundi ya kigaidi nchini Syria, alisema Erdogan, akisisitiza kuwa Rais wa Syria Ahmad Alsharaa atapambana dhidi ya makundi hayo.