Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan atakuwa mwenyeji wa Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier jijini Ankara siku ya Jumatano kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, kulingana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun.
Kikao hicho kinakuja wakati wa mabadiliko ya hali ya kisiasa katika eneo la Ulaya na Mashariki ya Kati, huku nchi hizo zikiwa mstari wa mbele katika kuleta amani ya kanda, sera za uhamiaji na ushirikiano wa kiulinzi.
Uturuki na Ujerumani zina uhusiano mzuri wa kihistoria, kiuchumi na kijamii huku Ujerumani ikiwa na raia wengi wenye asili ya Kituruki ulimwenguni.
Mazungumzo hayo pia yatagusia masuala ya ushirikiano kwenye sekta ya ulinzi, huku uhusiano zaidi baina ya nchi hizo mbili ukitawala mazungumzo hayo, alisema Altun siku ya Jumanne.
Pia, mazungumzo hayo yataangazia hadhi ya jumuiya Waturuki walioko Ujerumani, kitu ambacho kimekuwa kama daraja kati ya nchi hizo mbili.
"Tunaamini kuwa uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na Ujerumani utazidi kuimarika kupitia ziara hiyo," alisema Altun huku akisisitizia umuhimu mazungumzo ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao wanatarajiwa kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya na masuala mengine ya umuhimu, ambayo yataakisi ushiriki wa Uturuki na washirika wengine barani Ulaya katika masuala ya biashara, usalama na sera za uhamiaji.