Wakati wa majadiliano yao siku ya Jumatatu, viongozi hao wameweka msisitizo kwenye ushirikiano katika nyanja ya usalama, uchumi na ujenzi mpya wa Syria./Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa serikali ya mpito ya Syria Ahmed Alsharaa, wamekutana jijini Ankara, kama hatua ya kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kukuza utulivu wa kikanda.

Wakati wa majadiliano yao siku ya Jumatatu, viongozi hao wameweka msisitizo kwenye ushirikiano katika nyanja ya usalama, uchumi na ujenzi mpya wa Syria.

Kwa upande wake, Rais Erdogan alisisitiza namna Uturuki inavyoisaidia Syria, akisema kuwa, "Kama ambavyo hatukuwaacha ndugu zetu wa Syria wakati wa matatizo, ndivyo tutakavyoendelea kuwapa misaada stahiki katika kipindi hichi."

Rais Erdogan pia aligusia utayari wa Uturuki wa kuisaidia Syria kupata kujitawala akisema, "Msingi wa sera yetu kwa jirani yetu Syria umeifadhi umoja wa nchi hii." Erdogan pia aliongeza kuwa nchi hizo zimekubaliana kuchukua juhudi madhubuti kuhakikisha kuwa amani na utulivu unarejea Syria.

Kiongozi huyo wa Uturuki pia alisisitizia utayari wa Ankara katika kuisaidia Syria katika mapambano yake dhidi ya ugaidi akisema, "Tuko tayari kuisaidia Syria katika mapambano dhidi ya aina zote za ugaidi, iwe ni daesh au kundi la PKK/YPG."

Ushirikiano wa kiuchumi na wa kibinadamu

Kwenye masuala ya kiuchumi, Erdogan alisisitiza utayari wa Uturuki kusaidia ujenzi mpya wa Syria.

"Tuko tayari kusaidia ujenzi wa miji ya Syria iliyoharibiwa vibaya," alisema Erdogan.

Kwa upande wake, Rais Alsharaa alikubali mustakabali wa ushirikiano na Uturuki katika sekta mbalimbali, akiishukuru Ankara kwa msaada endelevu.

"Watu wa Syria hawatosahau ukarimu wa taasisi za Uturuki, nchi ya Uturuki na watu wake," alisema.

Aligusia matamanio ya Syria kufikia ushirikiano madhubuti katika eneo la uchumi na biashara, akisema, "Tungependa sana kushirikiana katika utamaduni, uchumi na nyanja ya biashara ili tufikie malengo yetu ya kimkakati."

Pia alisisitizia ushirikiano wa kiusalama, kama kipaumbele kikuu na kusema, "Moja ya malengo yetu ni kuwa na ushirikiano wa kiusalama."

Pia, aliongeza kuwa Syria inalenga kuongeza ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu.

Wito wa shinikizo dhidi ya Israeli

Alsharaa ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza shinikizo kwa Israeli ili irejee makubaliano ya mipaka ya kabla ya mwaka 1967.

Ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Uturuki na Syria

Erdogan aliielezea ziara ya Alsharaa kama mwanzo mpya wa uhusiano kati ya Uturuki na Syria.

"Huu ni mwanzo tu wa urafiki wa kudumu na ushirikiano kati ya nchi zetu," alisema Erdogan.

Viongozi wote wawili walionesha matumaini yao juu ya hatua za mataifa mbalimbali kuhakikisha usalama wa kanda. Erdogan alihitimisha kwa kusema, "Kwa mshikamano wa pamoja, ni imani yangu kuwa tutaweza kuwa na amani na utulivu bila kuwepo na ugaidi katika eneo letu."

Mkutano huo uliashiria mwanzo mpya wa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Syria na Uturuki, na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, na kutatua changamoto za kiuchumi kwa pamoja.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika