Viongozi mbalimbali ulimwenguni wameendelea kutuma salamu zao za rambirambi kwa serikali ya Uturuki kufuatia ajali ya moto wa hoteli uliouwa watu 76 na kujeruhi wengine 51.
Uturuki ilitangaza siku ya Jumatano kuwa siku ya maombolezo kitaifa kufuatia vifo hivyo katika hoteli moja iliyoko katika jimbo la Bolu, mapema Jumanne.
Umoja wa nchi za Kiturk ulipeperusha bendera zao nusu mlingoti kama ishara ya mshikamano na Uturuki.
“Tumesikitishwa na tukio hili na tunatuma salamu zetu za pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Tunawaombea nafuu ya haraka wale wote waliojeruhiwa katika tukio,” umesema umoja huo.
Rais wa Kazakh Kassym-Jomart Tokayev alituma salamu zake za rambirambi akiwaombea nafuu majeruhi wa tukio hilo.
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pia alituma salamu zake za rambi kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na watu wa Uturuki.
"Naomba nimtakie kila majeruhi nafuu ya haraka. Ukraine ipo katika majonzi na watu wa Uturuki katika kipindi hichi kigumu," alisema Zelenskyy kupitia mtandao wa X.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alionesha masikitiko yake kutokana na tukio hilo. “Mawazo yangu yapo pamoja na familia za waliopoteza wapendwa wao na niwatakie nafuu ya haraka majeruhi wa tukio hilo,” aliandika katika ukurasa wake wa X.
Nao Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ulituma salamu za rambirambi kwa serikali ya Uturuki, ikionesha mshikamano na jamhuri hiyo kufuatia janga la moto katika hoteli moja huko Bolu ambali pia limegharimu maisha ya watu na kuwaacha wengi na majeraha.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imetuma salamu hizo kwa watu wa Uturuki na serikali ya nchi hiyo, na pia kwa familia wa waathirika wa tukio hilo, ikiwaombea nafuu ya haraka majeruhi wa ajali hiyo ya moto.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki pia ilituma salamu zake za rambirambi kwa Uturuki kupitia ukurasa wake wa X, ikisema "Watu wa Uturuki wamekuwa nasi siku zote hasa katika nyakati ngumu na leo sisi Wasyria tunasimama na ndugu zetu wa Uturuki, katika kipindi hiki kigumu."
Kwa upande wake, China ilituma salamu zake za pole kwa waathirika wa tukio hilo na familia za walipoteza ndugu zao na kuwaombea majeruhi nafuu ya haraka.
Iran pia ilituma salamu za rambirambi kwa watu wa Uturuki. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa nchi amewaombea msamaha wa Mungu waathirika wa tukio hilo.
“Fikra zetu zipo pamoja na familia za wafiwa na wale wote walioathirika na janga hilo. Tunawaombea wote waliojeruhiwa nafuu ya haraka, alisema Rais wa Rwanda Paul Kagame kupitia ukurasa wake wa X.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje pia aliweka taarifa yake kwenye mtandao wa Facebook akionesha kusikitishwa na tukio hilo na kuwaombea nafuu ya haraka majeruhi wote.