Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier wametoa rai ya kuongezeka kwa juhudi za kimataifa za kusitisha mapigano huko Gaza na uwepo wa dola mbili katika mgogoro baina ya Israeli na Palestina.
Wakizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Ankara siku Jumatano, viongozi hao waliweka msisitizo kwenye nafasi ya diplomasia na kuonya dhidi ya hatua zinazolenga kudidimiza sheria za kimataifa.
Erdogan alisisitiza umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa karibu na kusitisha mapigano hayo ili kufikia suluhisho la kidiplomasia katika mgogoro huo.
"Kila mtu ana jukumu kubwa la kushikilia msimamo wa kusitisha mapigano huko Gaza. Kama jumuiya ya kimataifa, ni lazima tuendelee kushinikiza suluhisho la mataifa mawili," alisema Erdogan.
Rais huyo wa Uturuki alisema nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Ujerumani katika masuala muhimu mbalimbali, ikiwemo migogoro ya Gaza ya Palestina, Syria na Ukraine.
Steinmeier apinga mpango wa uhamishaji watu wa Gaza
Steinmeier alilaani vikali pendekezo la hivi karibuni la Rais wa Marekani Donald Trump, la kutaka “kuinyakua” Gaza na kuwahamisha raia wake kwenda nchi za jirani, akisema jambo hilo halikubaliki.
"Suluhisho kama hilo, ambalo linakiuka sheria za kimataifa halikubaliki, " alisema Steinmeier.
Pia alisisitiza kuwa amani ya kudumu ndio njia pekee ya kuipa ulinzi Israeli na kujiamini kwa Wapalestina.
"Steinmeier, ambaye kabla ya hapo alipata fursa ya kuzitembelea Saudi Arabia na Jordan, alisema kuwa viongozi mbalimbali ulimwenguni wamepinga mkakati huo.
"Nimesikitishwa na kukasirishwa na mpango wa Trump," alisema.
Kauli hiyo, ilitolewa na Trump wakati akiwa na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, imekosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa.
Baadhi ya nchi zilizochukizwa na kauli hiyo ni pamoja na Uturuki, Ujerumani, China, Urusi, Hispania, Ufaransa, Saudi Arabia na Misri.
Utulivu wa kanda na uhusiano wa Uturuki na Ujerumani
Mbali na Gaza, viongozi hao pia walijadiliana changamoto za mipaka, huku Erdogan akisisitiza umuhimu wa upatikanaji amani ya kudumu nchini Syria.
"Ni matamanio yetu kuona Syria yenye mafanikio na yenye amani," alisema.
Pia, alionesha kusikitishwa kwake kwa kuongezeka kwa matukio ya ubaguzi na ubaguzi dhidi ya Waislamu, hususani athari zake kwa jumuiya ya Waturuki.
Ziara ya Steinmeier jijini Ankara inakuja katika kipindi muhimu wakati kumekuwepo na ungezeko la shinikizo dhidi ya Israeli kusitisha mashambulizi yake huko Gaza.
Wakati huo huo, Uturuki na Ujerumani zimeendeleza jithihada za kidiplomasia ili kutatua migogoro ya kikanda na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili.