Uturuki na Indonesia wameimarisha ushirikiano wao wa kimkakati baada ya kutia saini makubaliano 13 katika nyanja mbalimbali ikiwemo ulinzi, vyombo vya habari na sekta nyinginezo.
Tukio hilo la Jumatano, lililofanyika Bogor, lilifuatiwa na Baraza la Ushirikiano la Ngazi ya Juu pamoja na mkutano na waandishi wa habari, uliomshirikisha Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Indonesia Prabowo Subianto.
Kati ya makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kiulinzi, ikiwemo mradi wa pamoja wa uzalishaji wa ndege nyuki za Bayraktar TB3 na Bayraktar AKINCI.
Mikataba hiyo ilitiwa saini na kampuni ya ulinzi ya Baykar na ile ya Indonesia iitwayo Republikorp, hatua inayolenga kudumisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili.
Katika hatua ambayo inalenga kuimarisha uwezo wa kiulinzi, Indonesia inalenga kuagiza ndege nyuki za Bayraktar TB3 na Bayraktar AKINCI na ndege zisizo na rubani kutoka Uturuki.
Wakati huo huo, mkataba wa pamoja kati ya Baykar na Republikorp ulisainiwa kwa malengo ya kukuza uzalishaji wa ndani wa vifaa vya ulinzi. Mkataba huo, ambao ulisainiwa na Meneja Mkuu wa Baykar Haluk Bayraktar, unalenga kusisitiza utayari wa nchi hizo mbili katika kubadilishana teknolojia.
Hatua hiyo ni mpango mkakati mwingine wa kujitania kwa Baykar.
Hivi karibuni, Baykar iliinunua kampuni ya anga ya Italia, Piaggio.
Pia, Baykar na Republikorp zimekubaliana kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa ndege zisizo na rubani huko Indonesia. Kiwanda hiko kipya kinalenga kuimarisha tasnia ya ulinzi ya Uturuki pamoja na kuwezesha uwezo wake wa teknolojia.
“Tunategemea makubwa kutoka ushirikiano huu, ambapo Uturuki itatoa uzoefu wa kutosha katika utengenezwaji wa ndege zisizo na rubani kwa manufaa ya Indonesia,” alisema afisa mmoja wa Uturuki.
Afisa huyo alionesha matumaini yake kuhusu ushirikiano huo, akiangazia uzoefu wa kiiteknolojia wa Uturuki katika uendeshwaji wa ndege zisizo na rubani.
Sekta ya biashara na uwekezeji pia zilipata msukumo baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano yenye kulenga kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya viwanda ulisainiwa na Waziri wa Viwanda na Teknolojia wa Uturuki Mehmet Fatih Kacir na Waziri wa Viwanda wa Indonesia Agus Gumiwang Kartasasmita.
Ushirikiano katika taaluma na nishati
Waziri wa Nishati na Maliasili wa Uturuki Alparslan Bayraktar na Waziri wa Nishati na Madini wa Indonesia Bahlil Lahadalia walitiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika nishati na maliasili.
Mikataba hiyo pia iliangazia mambo mengine kama vile kilimo, elimu, na dini. Waziri wa Kilimo na Misitu wa Uturuki Ibrahim Yumakli na mwenzake wa Indonesia Andi Amran Sulaiman, walitia saini mkataba wa ushirikiano katika kilimo.
Wakati huo huo, mkataba wa ushirikiano kati ya Baraza la Elimu ya Juu la Uturuki na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ya Indonesia, ulitiwa saini kwa lengo la kushirikiana katika tafiti na kukuza ushirikiano wa kitaluuma.
Masuala ya kidini pia yaliangaziwa kufuatia makubaliano kati ya ofisi ya Rais ya Uturuki inayoshughulikia masuala ya kidini, ikiongozwa na Ali Erbas, na Wizara ya Mambo ya Kidini ya Indonesia iliyowakilishwa na Nasaruddin Umar. Mkataba huo unalenga kukuza ushirikiano katika eneo hilo.
Ushirikiano wa huduma za afya na vyombo vya habari
Shirika la habari la Uturuki la Anadolu Agency na lile la Indonesia liitwalo Antara, yalikubaliana kuongeza ushirikiano katika taaluma ya uandishi wa habari.
Pia kulikuwa na mkataba wa ushirikino katika ya Shirika la Habari la Uturuki (TRT)na yale ya Indonesia ya LPP RRI na TVRI, yenye kulenga kubadilishana maudhui.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na mwenzake wa Indonesia Sugiono walitiliana mkataba wa ushirikiano katika sekta za afya na sayansi ya tiba.
Mikataba hiyo ya kihistoria ilidhihirisha ushirikiano kwa kiuchumi na kimkakati kati ya Uturuki na Indonesia.