Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amempongeza rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune kwa mafanikio yake katika uchaguzi wa rais.
Wakati wa simu siku ya Jumapili, Rais Erdogan alibainisha kuwa matokeo ya uchaguzi yanaonyesha uungwaji mkono mkubwa wa watu wa Algeria kwa hatua zilizopigwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Alionyesha imani kuwa utulivu na ustawi wa Algeria utaendelea kuimarika katika muhula mpya na kusisitiza imani yake kwamba uhusiano wa Uturuki na Algeria utaendelea kustawi katika nyanja zote, kwa namna inayolingana na uhusiano wa kindugu kati ya mataifa hayo mawili.
Rais wa sasa wa Algeria Tebboune ameshinda muhula wake wa pili wa urais wa miaka mitano katika uchaguzi wa mapema uliofanyika Jumamosi. Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, mkuu wa mamlaka ya uchaguzi ya Algeria alitangaza Jumapili kwamba Tebboune alishinda kwa asilimia 94.65 ya kura.
Rais Erdogan pia alimwalika Tebboune kutembelea Uturuki. Alipongeza juhudi za Algeria kama mjumbe wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono kadhia ya Palestina na kusisitiza uungaji mkono wa Uturuki kwa juhudi hizi.
Erdogan amesisitiza kuwa, nchi zote mbili zitaendelea kuzidisha juhudi za kukomesha mashambulizi ya Israel dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.