Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Iddi Seif Bakari amewasilisha barua yake kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika Ikulu ya Rais mjini Ankara. Picha: Ikulu ya Rais Uturuki.

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Iddi Seif Bakari amewasilisha barua yake rasmi kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika Ikulu ya Rais mjini Ankara.

Balozi Iddi Seif Bakari ambaye alikabidhiwa majukumu ya kuiwakilisha Tanzania nchini Uturuki baada ya awamu ya Balozi wa zamani wa Tanzania nchini humo, Luteni Jenerali Yakubu Hassan Mohamed kukamilika, alimkabidhi Rais Erdogan wa Uturuki nyaraka zake za ubalozi kwenye hafla fupi ya hali ya juu iliyoandaliwa Ikulu ya Ankara, Uturuki.

Balozi anatarajiwa kuendeleza uhusiano wa Uturuki na Tanzania baada ya kuapishwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Ikulu ya Chamwino, Dodoma mnamo tarehe 16 Juni, 2023.

Kabla ya uteuzi wake, Balozi Iddi Seif Bakari alikuwa Konseli Mkuu wa Tanzania. Dubai.

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Iddi Seif Bakari akimkabidhi barua yake rasmi Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Alhamisi.

Tanzania na Uturuki zimekuwa na uhusiano wa kihistoria uliodumu kwa miaka mingi baina ya raia wa nchi hizo na serikali hizo mbili.

Kwa upande wa biashara, Tanzania na Uturuki zimeshuhudia ufanisi mkubwa baina yao huku mauzo ya nje kutoka Uturuki kwenda Tanzania yakiongezeka kwa kiwango cha asilimia 17.3 kila mwaka kutoka dola milioni $4.55 mnamo 1995 hadi dola milioni 500, mwaka 2022.

Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Ndege la Uturuki, Turkish Airlines imechangia kuunganisha nchi hizo mbili kutokana na safari zake za mara tatu kwa wiki na za moja kwa moja kati ya Istanbul na mji wa Dar es Salaam na Zanzibar.

TRT Afrika