Waziri wa Spoti wa Somalia Mohamed Barre ameomba radhi kwa taifa baada ya Mwanariadha Nasro Ali Abukar kumaliza wa mwisho kwenye kitengo cha mita 100 katika mbio zilizofanyika uwanjani Shuangliu, China.
Nasro Ali Abukar, amegeuka kicheko cha kitaifa huku raia wa Somalia wakionyesha ghadhabu kwa matokeo yake alipomaliza wa misho katika mbio hizo.
Kilichozua hoja sio kumaliza mwisho kwa mwanariadha huyo anayesomea katika Chuo kikuu cha Jobkey nchini Somalia, bali kasi na mwendo wake uliomdhihirisha kuwa mshiriki asiyehusika kwenye riadha au mwanariadha bila mazoezi tofauti na wanariadha wenzake.
"Kwa kweli, yaliyotokea ni aibu kwa bendera ya nchi na jamii ya Wasomali. Kama wizara, tunasikitika sana na tunaomba msamaha kwa jamii nzima ya Wasomali. Wizara ya michezo haifahamu jinsi alivyochaguliwa kuliwakilisha taifa." Waziri Bare alisema.
Aidha, waziri huyo amekana kuhusika kwa wizara yake au kufuatwa kwa taratibu katika uteuzi wa wanariadha huyo kushirki kwenye michezo ya dunia ya vyuo vikuu FISU vinavyoendelea mjini Chengdu, China.
"Tumegundua kuwa uteuzi uliofanywa ni wa kitapeli. Maafisa wa mashirikisho ya michezo wanapaswa kuwachagua wanariadha ipasavyo na nitawachukulia hatua chama husika kilichowapelekea wanariadha nchini China." Ameongeza Waziri.
Hata hivyo, mwakilishi mwingine wa Somalia katika mbio hizo Hassan Ali Idow amefanya vyema na kufuzu kwa fainali za kitengo cha mita 1500.