Somalia imeeleza kuwa uchunguzi wa pamoja wa Kamati ya olimpiki, bodi ya utendaji ya shirikisho la riadha, na wizara ya riadha juu ya ushiriki wa Somalia kwenye mashindano ya kimataifa ya vyuo vikuu, FISU, umebaini kuwa mkimbiaji aliyeshiriki mbio hizo ni mpwa wa aliyekuwa mkuu wa riadha nchini humo, Khadija Aden Dahir.
Kufuatia sakata hiyo, shirikisho la riadha la Somalia, limemsimamisha kazi Khadija na kuunga mkono hatua za wizara ya michezo nchini Somalia na kamati ya Olimpiki nchini humo kumchukulia hatua za kinidhamu Khadija Aden Dahir.
Shirikisho la riadha Somalia SAF, limeongeza kuwa rais huyo aliyeondolewa wa shirikisho hilo, Khadija Aden Dahir alisafiri na dada yake na mpwa wake kama wawakilishi wa Somalia.
Kutokana na tabia isiyokubalika ya upendeleo na matumizi mabaya ya madaraka, bodi ya utendaji ya shirikisho la riadha la Somalia imemsimamisha Khadija kwa mujibu wa katiba ya SAF.
Waziri wa michezo Somalia Mohamed Bare amekaribisha hatua ya Shirkisho la riadha dhidi ya Khadija.
"Ninakaribisha uamuzi wa kumsimamisha kazi Khadija Aden Dahir. Hatua Hii ilikuwa muhimu kufuatia tukio la michezo ya vyuo vikuu duniani vya FISU. Wizara inatambua umuhimu mkubwa wa uwajibikaji katika kukuza uadilifu na usawa katika nyanja ya michezo." Waziri Bare alisema.

Shirkisho la riadha Somalia, SAF, limeongeza kuwa; "Hatua hii ni muhimu kwa maslahi ya wanariadha wa Somalia ambao ndio sehemu kuu ya SAF, wanaojiandaa kwa michezo ya kimataifa ikiwemo ubingwa wa dunia mjini budapest mwishoni mwa Agosti, michezo yote ya Afrika na michezo ya Olimpiki ya paris 2024.
Aliyekuwa naibu rais wa Shirkisho la riadha Somalia, SAF, Farah Ali Moallin ametuliwa kuwa Kaimu rais wa Shirikisho hilo.