Felix Tshisekedi akiwapokea wachezaji wa DRC katika Ikulu ya nchi hiyo, mjini Kinshasa. /Picha:Ikulu DRC

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amekipokea kikosi cha timu ya taifa ya DRC kilichorejea nchini humo baada ya ushiriki wao katika michuano ya AFCON 2023, nchini Ivory Coast.

"Nyinyi ni timu ya vijana ambao hamkupata muda wa kutosha kujiandaa, hata hivyo mmeonyesha vipaji vyenu hata kuwashangaza wengi, kwani hakuna aliyetarajia ninyi kufika hatua hii ya mashindano. Nina hakika kwamba mtafanya maajabu tena," alisema Rais Tshisekedi.

"Ni heshima kubwa kwangu kuzungumza kwa niaba ya taifa zima na kuwashukuru kwa kuleta furaha kwa Wakongo," alisema.

Rais Tshisekedi pia alikaribisha ishara iliyooneshwa na wachezaji wa Kongo wakati wimbo wa taifa lao unapigwa, kwenye mechi iliyowakutanisha na wenyeji, Ivory Coast.

Hii ni baada ya wachezaji wote wa DR Congo kuonesha ishara ya kuziba midomo yao huku na kuelekeza vidole viwili kwenye vichwa vyao, wakionesha mshikamano na kuziari jumuiya za kimataifa kuchukua hatua dhidi ya hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

"Hata mkiwa mbali na nchi, mlishikamana na wananchi wenzenu. Kongo haitosahau kamwe, " alisisitiza.

"Kazi lazima iendelee kwa sababu tuna changamoto mbili kubwa mbele yetu."DRC lazima iwe na sifa AFCON Morocco 2025, ambayo mechi za kufuzu zitaanza hivi karibuni, na Kombe la Dunia FIFA 2026," Waziri wa Michezo, Kabulo Mbwana Kabulo ambaye pia alikuwepo kwenye hafla hiyo, alisema.

DRC ilimaliza katika nafasi ya nne, katika makala ya 34 ya AFCON 2023, nyuma ya Afrika Kusini (3), Nigeria (2) na mabingwa Ivory Coast.

TRT Afrika